Home Kitaifa TBS YATOA VYETI NA LESENI ZA UBORA 2,402, WAJASIRIAMALI WADOGO WAKIWA 1,066.

TBS YATOA VYETI NA LESENI ZA UBORA 2,402, WAJASIRIAMALI WADOGO WAKIWA 1,066.

Mkurugenzi Mkuu Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt Ashura Katunzi ameeleza kuwa jumla ya vyeti na leseni za ubora 2,402 vimetolewa kwa wazalishaji, miongoni mwao wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,066.

Na pia Serikali kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya sh. milioni 350 kila mwaka kwa madhumuni ya kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote ambapo Leseni hizi zimesaidia wazalishaji kuweza kuzalisha bidhaa bora, ikiwa ni pamoja na bidhaa zao kuweza kuaminika sokoni na pia kufanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Dkt Katunzi amesema hayo leo hii Machi 18,2025 Jijini Dodoma akizungumza na Wanahabari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.

Aidha Dkt Katunzi amesema katika kipindi hicho Shirika limeendelea na huduma za usajili wa maeneo ya uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula na vipodozi kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wa maeneo hayo ili kuendelea kulinda afya za walaji ambapo jumla ya maeneo 31,592 yalisajiliwa. Na pia katika kuimarisha ukaguzi wa bidhaa mbalimbali zinazoingia nchini kutoka nchi za nje, TBS huhakiki ubora wa bidhaa na magari yaliyotumika kabla ya kusafirishwa kuja nchini ambapo kwa kipindi cha miaka hiyo jumla ya shehena za bidhaa 18,588 zilikaguliwa, sanjari na magari 162,160. ambapo bidhaa hizi zinakaguliwa kwa lengo la kuiepusha Tanzania kuwa jalala la bidhaa duni pamoja na kulinda afya, usalama na mazingira ya watumiaji.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilianzishwa kama sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya sekta za Viwanda na Biashara ili kukuza uchumi wa Taifa na linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria ya Viwango Sura 130.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!