Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo amelipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa utendaji mzuri na kulitaka kuongeza nguvu katika utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara hususani upatikanaji wa nembo ya ubora wa bidhaa ili kukuza biashara, kuongeza ajira, Pato la Taifa na uchumi kwa ujumla.
Ameyasema hayo Julai 11, 2024, Ubungo jijini Dar es Salaam alipotembelea TBS kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika hilo ili kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi wa Shirika hilo katika kuwahusumia wafanyabiashara.
Aidha, ametoa wito kwa Watumishi wa Shirika hilo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na ushirikiano baina yao pamoja na kuepuka kuwa kikwazo katika utoaji huduma kwa wafanyabiashara ili kuiwezesha sekta binafsi kukua kwa kasi na kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga uchumi shindani wa viwanda.
“Lengo la Wizara ya Viwanda na Biashara ni kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wafanyabiashara ili waweze kufanya biashara zao kikamilifu, kuongeza ajira na kukuza Pato la Taifa kupitia Taasisi zake 13 ambazo tutaanza kuzipima kulingana na utendaji kazi wake“. Amesema Dkt. Jafo.
Dkt. Jafo pia ameielekeza TBS kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) pamoja na taasisi nyingine katika kuhakikisha Wajasiriamali wengi wanapata nembo ya ubora na kufuatilia biashara hizo ili kuhakikisha kiwango cha ubora wa bidhaa hizo haushuki kwa ajili ya kuwalinda walaji.
Akitoa mfano wa kuweka virutubisho kwenye vyakula kama unga wa mahindi, ngano na mafuta ya kula, Dkt Jafo amesema TBS inajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa Viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo zinazostahili kuwekewa virutubisho, wanaweka virutubisho hivyo kwa usahihi ili kuwalinda wananchi kuwa na afya njema na kuwaepusha kupata udumavu ambao unaweza kuwa na madhara makubwa katika ujenzi wa uchumi imara.
“Ni muhimu sana kuwalinda Wananchi kwa kupata bidhaa zenye ubora na viwango vinavyotakiwa kulingana na gharama ya bidhaa hizo.” Amesema Dkt. Jafo.