-Ujenzi wa madaraja kwenye
mito kuwaepushia vifo wananchi
Kilosa
Imeelezwa kwamba ndani ya kipindi kifupi kumekuwa na maendeleo katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi katika maeneo ya vijijini na mijini hii inatokana na kazi kubwa ilivyofanywa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunganisha barabara za mijini na vijijini ikiwemo maeneo ya masoko pamoja na maeneo ya uzalishaji.
Hayo yameelezwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mhe. Denis Londo wakati akielezea utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofanya na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilayani Kilosa.
Mhe. Londo amesema kuwa kazi kubwa imefanyika Mikumi na kwa mafanikio makubwa ujenzi wa daraja la Ruhembe lenye urefu wa mita arobaini kukamilika kwake litasaidia kuwaondolea adha ya usafiri wananchi wa eneo hili waliyokuwa nayo kwa muda mrefu wakiwemo wajawazito na wagonjwa waliokuwa wakienda kupata huduma mbalimbali ng’ambo ya mto huo.
“Daraja hili ni muhimu sana kwa maisha ya wakazi wa Bonde la Ruhembe, kata za Kidodi na Ruaha kwa sababu linaenda kuwapunguzia umbali kutoka kilomita 32 walizokuwa wakizunguka hapo awali mpaka kilomita 2 kutoka barabara kubwa kwenda kijijini, pia eneo hili ni mabondeni hivyo wakati wa mvua barabara zilikua hazipitiki kabisa na kusababisha akiba ndogo ya mkulima kutumika sana kwa ajili ya usafirishaji wa pembejeo za kilimo na kukamilika kwa daraja hili linaenda kupiga vita adui umasikini” Amesisitiza Mhe. Londo.
Kwa upande wa barabara Mbunge huyo amesema barabara ya kilomita tano kutoka Kidodi kwenda Kidunda imekamilika ambapo kijiji hicho cha Kidunda hakikuwahi kupata barabara tangia uhuru ”Milima ya Kidunda ndio ilikua ikilisha eneo kubwa la mkoa hivyo sasa hivi uzalishaji umeongezeka kwani sasa mazao yote yanasafirishwa kwa usafiri mbalimbali na hivyo tunaweza kuona miundombinu hiyo inavyoleta maendeleo na uwekezaji unaongezeka”.
Aidha, amesema barabara ya kilomita 42 kutoka Ulaya kwenda Kisanga upande wa Kilosa ambayo ilikua haipitiki takribani miaka 20 na sasa inaenda kukamilika na kuunganika kwa barabara hiyo inaenda kumpunguzia mwananchi umbali wa zaidi ya kilomita 75 ambapo alikua akitumia saa tatu na hivyo kukamilika kwa barabara hiyo mwananchi ataenda kutumia nusu saa kufika pia kukosekana na barabara hiyo ilisababisha vifo vingi kwani watu wengi walikua wanachelewa kupata huduma muhimu hususani huduma za afya.
Amesema sasa hivi jimbo la Mikumi linaenda kuunganishwa na ndio fahari kwa wananchi kwani Serikali ya Awamu ya Sita inaenda kutatua kero kwa wananchi”Kila mmoja anaguswa na hii miradi ya TARURA kwani inashiriki kikamilifu kwa kuhakikisha miundombinu wanayojenga inawagusa kila mwananchi na hivyo kuinua uchumi kwa kuongeza tija katika uzalishaji”.
Hatahivyo amewataka wananchi kulinda miundombinu ya barabara isiharibike ili kuifanya Serikali kuweza kupeleka maendeleo sehemu nyingine kwakuwa wajibu wa mwananchi ni kulinda miundombinu na kuifanya serikali kutumia fedha zake kwa maendeleo mengine.
Naye, Diwani wa Kata ya Ulaya Mhe. Ally Kibati ameishukuru TARURA kwa usimamizi mzuri wa kukamilisha barabara na ujenzi wa Box karavati la Ulaya-Kisanga ambapo kwa muda mrefu wananchi walikuwa wakipata changamoto nyingi hususani za kusafirisha mazao yao lakini hivi sasa barabara imefunguka na hivyo kuwapunguzia gharama za usafirishaji.
Wakati huo huo Mkazi wa Kata ya Ulaya Steven Mahanga ameipongeza Serikali kwa kuwaletea mradi wa ujenzi wa Box karavati la ulaya-kisanga kwa sababu awali kulikuwa kunatokea mauaji mengi kutokana na kukatika kwa barabara na hivyo kama raia wapo tayari kuilinda miundombinu hiyo ili kupata maendeleo zaidi katika kata yao.
-Mwisho-