

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumapili, Machi 9, 2025, anatarajiwa kuwa mkoani Kilimanjaro, ambapo pamoja na mambo mengine, atakuwa katika eneo la Nyumba ya Mungu, wilayani Same, kuzindua Mradi wa Maji Same-Mwanga-Korogwe.
Mradi wa maji Same-Mwanga-Korogwe ulisanifiwa mwaka 2008, ambapo serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Arab Bank for Economic Development in Africa na wadau wengine, ililenga kujenga mradi mkubwa wa maji kwa ajili ya kuhudumia wakazi wa miji ya Same na Mwanga pamoja na vijiji 38 vya Wilaya ya Korogwe ili kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Mradi huu umetumia takribani shilingi bilioni 300 kwa awamu ya kwanza, na kwa sasa kazi zinazoendelea ni pamoja na Kuendeleza mtandao wa mabomba na kufanya maunganisho ya maji kwa wananchi.
Kukarabati na kuboresha miundombinu chakavu ya maji, ikiwa ni pamoja na kubadilisha mabomba makubwa ili yaendane na mahitaji ya sasa.

Inatarajiwa kuwa ifikapo Aprili 2025, huduma ya maji itakuwa imewafikia wananchi walengwa kwa asilimia 95.
Kukamilika kwa mradi huo wa maji, kunatajwa na serikali kuwa kutapelekea upatikanaji wa maji ya kutosha katika miji ya Same na Mwanga, hivyo kutoa fursa kwa wawekezaji kuchangia kukuza uchumi wa maeneo hayo na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla. Upatikanaji wa maji utakuwa wa uhakika kwa saa 24, tofauti na awali ambapo maji yalipatikana kwa muda wa saa sita pekee kwa siku.
