Na Benny Mwaipaja, New York
Netherlands imeahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo utekelezaji wa miradi ya kimkakati itakayo changia kukuza maendeleo ya nchi na watu wake
Ahadi hiyo imetolewa jijini New York nchini Marekani na Naibu Waziri wa Mambo ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Netherlands Mhe. Steven Collet, alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba, Kando ya Mikutano ya Jukwaa la Juu la Siasa ya Umoja wa Mataifa inayojadili tathimini na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.
Mhe. Collet aliahidi kuwa Serikali yake itaongeza ufadhili kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ya kilimo, nishati, uongezaji thamani wa madini, kusaidia wajasiriamali wadogo pamoja na ujenzi wa baadhi ya miundombinu ambayo Serikali inatekeleza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba, ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, aliishukuru Netherlands kwa ushirikiano wa kimaendeleo inayotoa kwa Tanzania ikiwemo kusadia utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kupitia Umoja wa Ulaya (EU)
Alisema kuwa Tanzania ina mengi iliyonufaika kutoka Natherlands ikiwemo ufadhili wa miradi ya kilimo, afya, elimu na mingine kadha wa kadha inayotekelezwa na Sekta binafsi na kwamba ushirikiano huo utaendelea kuzinufaisha pande zote mbili.
Aliiomba Netherlands kuisaidia pia Tanzania kufikia masoko ya fedha kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa njia ya kuuza hewa ukaa, ambayo ni biashara kubwa duniani hivi sasa na kwamba Tanzania ina sifa za kunufaika na mpango huo kwa kuwa ina rasilimali nyingi zinazotakiwa kuhifadhiwa na kuiingia nchi fedha za kigeni.