Home Biashara TANZANIA KUZIDI KUNUFAIKA NA MIRADI YA WIPO

TANZANIA KUZIDI KUNUFAIKA NA MIRADI YA WIPO

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa Jijini Geneva Uswisi, Mhe. Balozi Maimuna Tarishi amesema kuwa Tanzania inaendelea kunufaika na miradi mingi ambayo hutolewa na Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO).

Kauli hiyo aliitoa alipotembelea ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) tarehe 22 Novemba, 2022 ili kujionea namna taasisi inavyotekeleza majukumu yake. Mhe. Balozi pia alipokea taarifa za utekelezaji wa shughuli na miradi inayofanyika kwa ushirikiano baina ya Tanzania na WIPO, BRELA ikiwa ni msimamizi mkuu wa majukumu ya miliki ubunifu nchini.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Bw. Andrew Mkapa akimkaribisha katika ofisi za BRELA amebainisha majukumu ya Taasisi kisheria na namna ambavyo BRELA inashirikiana na WIPO kwa karibu kutokana na utekelezaji wa jukumu la miliki ubunifu nchini Tanzania.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu, Bi. Loy Mhando amemshukuru Mhe. Balozi Tarishi kwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia masuala ya Miliki Ubunifu na kuwa kiungo kati ya Tanzania na WIPO na kumueleza kuwa baada ya mkutano wa 63 wa WIPO uliofanyika mwezi Julai, 2022 Geneva-Uswisi, BRELA imeanza kutekeleza maeneo ya mashirikiano, hivyo kuiomba ofisi yake kutoa usaidizi wa karibu wa kufuatailia masuala yanayowasilishwa WIPO.

Bi. Mhando amebainisha maeneo yanayohitaji usaidizi kutoka ofisi yake ni pamoja na rasimu ya Sera ya Miliki Ubunifu ya Taifa kwa ajili ya kupata usaidizi wa kitaalamu ili kuboresha nyaraka hiyo kwa kuwa WIPO ni wabobezi wa masuala ya Miliki Ubunifu.

Vilevile, amemuomba anapokutana na Mkurugenzi Mkuu wa WIPO kuwasilisha uhitaji kuwajengea uwezo watumishi na watumiaji wa Miliki Ubunifu ili waweze kusimamia na kutumia Miliki Ubunifu kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Aidha, amemueleza Mhe. Balozi kuwa, Tanzania kupitia WIPO imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali zinazofanyika kwa ushirikiano ikiwemo kuwezesha matumizi ya Miliki Ubunifu kwa wafanyabiashara na wabunifu; programu ya shahada ya uzamili inayotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kishirikiana na ARIPO, BRELA na WIPO na tathmini ya miliki ubunifu katika biashara; nk.

Bw. Mkapa amehitimisha kwa kumuomba Mhe. Balozi Tarishi kuishirikisha BRELA katika fursa mbalimbali zinazojitokeza katika mashirika ya kimataifa kwani BRELA ipo tayari kushirikiana na Ofisi yake kikamilifu kwa ajili ya mafaniko ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!