Na. Mathias Canal, WEST-Dar es salaam
Tanzania na Afrika Kusini zinarajiwa kusaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano katika maswala ya elimu msingi siku ya Maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani tarehe 7 Julai ambapo kitaifa yatafanyika Jijini Dar es salaam.
Kati ya makubaliano hayo yatakayowezesha kuimarisha ushirikaino kwa nchi hizo mbili ni pamoja na Tanzania kuisaidia Afrika Kusini kufundisha lugha ya Kiswahili.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 4 Julai 2021 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu ya Msingi wa Afrika Kusini Mhe Matsie Angelina Motshekga katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano (JNICC) Jijini Dar es salaam.
Akizungumza mara baada ya Mazungumzo hayo Waziri Mkenda amesema kuwa mkataba huo wa makubaliano unasainiwa ikiwa ni kutekeleza ahadi ya viongozi wakuu ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan na Rais wa Afrika Kusini Mhe Cyril Ramaphosa waliyoitoa ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu.
Waziri Mkenda amesema kuwa mara baada ya kusainiwa makubaliano hayo viongozi wakuu watakutana kwa ajili ya kuweka mpango kazi wa utekelezaji ili isiwe ni makubaliano pekee pasina utekelezaji wake.
Waziri huyo wa Elimu wa Afrika Kusini anatazamiwa tarehe 5 Julai 2022 kutembelea shule ya msingi ya Uhuru Mchanganyiko kadhalika kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe Balozi Liberata Mulamula pamoja na kukutana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Lela Mohamed Mussa.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu ya Msingi wa Afrika Kusini Mhe Matsie Angelina Motshekga amesema kuwa Afrika Kusini ina mtazamo mkubwa na Tanzania kubadilishana uzoefu katika udhamini wa mafunzo (Scholarship), kufanya kazi kwa pamoja na kubadilishana uzoefu katika sekta nzima ya elimu.
Mhe Motshekga amesema kuwa amekuja kusaini makubaliano hayo kwani yatakuwa muhimu na yenye tija kwa Tanzania pamoja na wananchi wa Afrika Kusini ambao wanaipenda na kuithamini lugha ya Kiswahili.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi amesema kuwa baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo bado Tanzania itaendelea kutumia fursa za kufundisha Kiswahili katika maeneo mengi.