Home Kitaifa TANGAZENI MAPITO YA MUUNGANO KWA ZAWADI ZA VITABU – SAMIA

TANGAZENI MAPITO YA MUUNGANO KWA ZAWADI ZA VITABU – SAMIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaelekeza Viongozi pamoja na Watanzania kwa ujumla kugawa vitabu vinavyoeleza mapito ya Muungano kama zawadi kwa viongozi na wageni wa nchi za nje.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zuhura Yunus imeeleza kuwa Rais Samia ametoa kauli hiyo leo wakati akizindua vitabu vya Miaka 60 ya Historia ya Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Kitabu cha Safari za Picha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka 60 kwenye hafla iliyofanyika Ikulu, Chamwino.

Aidha, Rais Samia amesema vitabu hivyo ni kumbukumbu muhimu kwa taifa na kwa Watanzania kwa kuwa watasoma na kupata taarifa mbalimbali ambazo hazipatikani kirahisi sehemu nyingine.

Rais Samia pia amesema vitabu hivyo vitawawezesha kukuza ujuzi na kujiongezea maarifa kuhusu Muungano wetu adimu na adhimu pamoja na kutunza historia inayoweza kutumika katika mambo kadhaa ikiwemo utalii.

Vile vile, Rais Samia amewasihi Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa letu, kufanya kazi kwa bidi na kudumisha uzalendo kwa kuuenzi kwa vitendo Muungano na Waasisi wake.

Uzinduzi wa vitabu hivyo ni sehemu ya shamrashamra ya sherehe za Muungano ambapo awali Rais Samia aliwatunuku Nishani za Muungano viongozi mbalimbali waliopo madarakani pamoja na wastaafu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!