Home Kitaifa TANESCO WAMEWASHA UMEME KISIWA CHA CHOLE WILAYANI MAFIA KWA MARA YA KWANZA

TANESCO WAMEWASHA UMEME KISIWA CHA CHOLE WILAYANI MAFIA KWA MARA YA KWANZA

Naibu Waziri wa Elimu sayansi na teknolojia na Mbunge wa Jimbo la Mafia Omari Kipanga ameongoza wananchi wa kisiwa cha Chole kuwasha umeme baa baada ya TANESCO kupitishwa Waya chini ya bahari ambako kwa mara ya kwanza baada ya kisiwa hicho kukosa huduma hiyo ya umeme tangu Mungu alipoumba kisiwa hicho.

Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Pwani limewasha rasmi umeme katika kisiwa cha Chole kilichopo kata ya Jibondo Wilayani Mafia kufuatia kukamilika kwa mradi uliotekelezwa kwa muda wa mwaka mmoja.

Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Shule ya msingi Chole wilayani Mafia na kuhudhuriwa na Wananchi, Viongozi mbalimbali wa CCM, Viongozi wa serikali ikiwa ni pamoja na timu ya TANESCO mkoa wa Pwani wakiwa wameongozwa na Meneja wa TANESCO mkoa wa Pwani Eng. Cosmas Mkaka.

Mradi huo ulioanza kutekelezwa kuanzia Julai 2023 unatarajiwa kusambaza umeme katika visiwa vingine vilivyobaki vya Juani na Jibondo kwa hatua nyingine na kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 3.2 hadi utakapokamilika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, mgeni rasmi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mafia na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omar Kipanga amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi.

” Tumshukuru Mhe. Rais kwa kukubali kutoa fedha pamoja na kuziimarisha taasisi zake ili kusimamia mradi huu” alisema Mhe. Kipanga. ” Tunawashukuru pia TANESCO na Mkandarasi wetu kwa kusimamia vizuri mradi na kukamilika kwa wakati, inabidi tuwe walinzi wa kwanza wa miundombinu hii ya umeme ili itunufaishe sisi na vizazi vingine” alieleza.

Ili kufanikisha sherehe hiyo Meneja wa Kampuni ya Nakuroi Investment Company Limited ambaye ndio aliyehusika kuvusha umeme huo alitoa ng’ombe mmoja dume kwaajili ya mboga.na Uongozi wa TANESCO wilaya ya Mafia kutoa kilo 200 za mchele huku mziki ukikesha mpaka asubuhi.

Umeme huo umegharimu zaidi ya shillingi Bililoni 3.2 zilizotokana na fedha za ndani.

Awali Mheshimiwa Kipanga alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa fedha alizotoa kufanikisha kufikisha umeme katika kisiwa hicho cha Chole .

Naye Meneja wa TANESCO mkoa wa Pwani Eng Cosmas Mkaka aliwataka Wananchi kila mmoja anakuwa mlinzi wa miundombinu ya umeme huo.

Lengo la mradi huo ni kuhakikisha kwamba kaya zaidi ya 1000 katika vijiji vyote vitatu vinaunganishwa umeme pindi utakaposambazwa kote.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mafia Abdul Kitungi amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa fedha zaidi ya shillingi Bililoni 3.2 za utekezaji wa mradi huo kwaajili ya kuhudumia Wananchi wa kisiwa cha Chole.

“Sasa hivi tunashukuru kwa kufika umeme kisiwani kwetu maana kabla ya kupata umeme tulikuwa na matatizo mengi, ila kwa sasa tunaamini biashara zitaongezeka na huduma za afya na shule zitakuwa vizuri, tunaishukuru sana Serikali kwa hatua hii” alisema kwaniaba ya wakazi wa kijiji cha Chole.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha chole, Ally Mgeni ameshukuru kwa hatua hiyo na kueleza umuhimu wa upatikanaji wa umeme kwa kuimarisha huduma za kiuchumi na kijamii zikiwemo Afya, na Elimu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!