Home Kitaifa TAMWA YATOA TAMKO KATIKA KUADHIMISHA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KINGONO

TAMWA YATOA TAMKO KATIKA KUADHIMISHA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KINGONO

Na Magreth Mbinga

TAMWA ilibaini kuwa tatizo kubwa la rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono mahala pa kazi na katika elimu ya vyuo vikuu sambamba na matokeo ya tafiti na uchapishaji wa habari kuhusu rushwa ya ngono yaliyochagiza wadau na waathirika kuweka wazi hali halisi ya rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono katika mazingira ya kazi na elimu.

Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dk Rose Reuben katika Mkutano na waandishi wa habari wakati akitoa tamko la kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

“TAMWA kwa kushirikiana na wanamtandao wa kupinga ukatili wa jinsia hapa Nchini pamoja na wadau wetu wa maendeleo kwanza tunajisikia fahari kuibua mengi kuhusu athari ya rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono mahala pa kazi na katika taasisi za elimu na kwa kuendeleza mjadala huu katika jamii kupitia vyombo vya habari”amesema Dk Reuben.

Pia Dk Reuben amesema TAMWA na WFT wanaiomba Serikali kuchukulia uzito suala la ukatili wa ngono na iendelee kuwawajibisha wale wanaoomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi na wafanyakazi .

“Tunapoadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia TAMWA tunatamani kuwa asiwepo yeyote au popote pale atakayefanyiwa ukatili wa kijinsia hapa Nchini rushwa ya ngono mahala pa kazi,vyuoni na mashuleni ni janga na inarudisha nyuma maendeleo ya jamii yetu”amesema Dk Reuben.

Aidha Mwanachama wa Men Engage Tanzania Dk Katanta Razalos Simwanza amesema rushwa ya ngono ni changamoto katika jamii hivyo inahitajika kupaza sauti kukemea vitendo hivyo ambavyo vinadhalilisha na kuondoa utu wa mtu.

“Kama wanaume wajibu wetu kukagua vyeti na sio maungo pale ambapo watu wanakuja kuomba kazi hasa wanawake tukikagua maungo tunadogosha utu wa mtu na tusisite kuwawajibisha wale wote wanao omba rushwa ya ngono”amesema Dk Katanta .

Sanjari na hayo Mratibu wa Kitaifa WILDAF Wakili Msomi Dk Anna Kulaya amesema vijana wengi wanalalamika kwamba hawana sehemu ya kupeleka malalamiko yao pindi wanapofanyiwa ukatili wa kingono.

“Tunatamani kuona vyuo vikuu na vyuo yva kati Nchi nzima vinafungua madawati ya kupinga ukatili wa kijinsia,wito wetu kwa Serikali iharakishe na iridhie mkataba wa kupinga rushwa ya ngono mahala pa kazi ili iweze kiwalinda wanawake na wanaume ambao wanafanyiwa ukatili”amesema Dk Kulaya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!