Home Kitaifa TAKUKURU PWANI WAJA NA MKAKATI MPYA KWA MWAKA 2023

TAKUKURU PWANI WAJA NA MKAKATI MPYA KWA MWAKA 2023

Na Magreth Mbinga

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Mkoa wa Pwani inashukuru Wananchi wa Mkoa huo kwa kuipatia ushirikianao kwa kipindi cha mwaka 2022 ambapo waliwezakufanya kazi kwa ukaribu zaidi na taasisi hiyo na kuiwezesha kutimiza majukumu yake kwa uweledi wa hali ya juu.

Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Ndugu Christopher Myava katika mahojiano na Mwandishi wetu yaliyo lenga mafanikio ya Taasisi hiyo kwa mwaka uliopita wa 2022 na mikakati ya mwaka 2023.

Myava amesema kwa mwaka 2022 walifanikiwa kufungua kesi 32 baada ya uchunguzi wao kukamilika na kuzifikisha kwa muendesha mashitaka ili waendelee na hatua zinazofata kuweza kuwachukulia hatua watuhumiwa wa vitendo vya rushwa .

Kwa kipindi cha mwaka 2022 Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Mkoa wa Pwani na Wilaya zake zote zilifanikiwa kupambana na rushwa kwa kushirikiana na Wananchi Kama tunavyojua kupambana na rushwa sio jukumu la Taasisi pekee bali ni mapambano ambayo yanatakiwa kuhusisha watu wote yani kila Mwananchi anajukumu la kupambana na rushwa mahali popote pale alipo” amesema Myava.

Pia Myava amesema mwaka huu wa 2023 ambao umeanza wanakuja na Programu mpya kwa Wananchi ambayo inaitwa TAKUKURU rafiki ambapo itawaleta Wananchi karibu kabisa na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa lengo ikiwa ni kuongeza wigo wa Wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.

“Taasisi itatilia mkazo zaidi katika programu hii ya TAKUKURU rafiki,kama inavyofaamika Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa mara nyingi imekuwa ikiendesha programu mbalimbali lengo ni kuhakikisha kwamba kila Mwananchi anashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa” amesema Myava.

Aidha Myava amesema programu hiyo itaendeshwa kwa njia ya vikao kuanzia ngazi ya kata ambapo itashirikisha Wananchi ambapo wataibua matatizo ambayo yapo katika maeneo husika mfano Idara ya afya,elimu au kuna Ujenzi unaendelea ambao haupo sawa pamoja na vitu vingine .

“Wananchi wakishaibua kero tutaijadili pamoja nao na kukubaliana namna ya kuweza kushughulikia na sisi kama Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa tunahakikisha kero hiyo inatatuliwa lakini kwa ushirikiano na Wananchi ambao wa ndio wenye jukumu la kuhakikisha maendeleo yanapatikana” amesema Myava.

Sanjari na hayo Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa itaendelea na majukumu yake kama kawaida kwa mwaka huu 2023 ikiwemo ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa lengo la kuhakikisha pesa ya Serikali inatumika kikamilifu na miradi yote inayotekelezwa Mkoa wa Pwani inapitiwa na Taasisi.

“Kama munavyofahamu Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dk Samia Suluhu Hassan imetoa pesa nyingi sana kuelekea katika nyanja mbalimbali lengo ni kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora sisi jukumu letu ni kuangalia pesa zinatumika kikamilifu ili kusiwe na mianya ya kuvujisha pesa hizo na kuweza kuwanufaisha watu wachache na kunufaisha Wananchi kwa asilimia kubwa” amesema Myava.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!