Home Kitaifa TAKUKURU MKOA WA TANGA YABAINI USAJIRI WAGONJWA HEWA WA VVU 313 WILAYA...

TAKUKURU MKOA WA TANGA YABAINI USAJIRI WAGONJWA HEWA WA VVU 313 WILAYA YA MUHEZA.

Na Boniface Gideon, TANGA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) mkoa wa Tanga imefanikiwa kudhibiti wagonjwa hewa 313 wa VVU Waliokuwa Wamesajiriwa na Wataalamu wa Afya kwenye mfumo wa usajili wa wagonjwa hao wilayani Muheza.

Hayo yalibainishwa leo Novemba 2 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga Zainabu Bakari wakati akizungumza na Waandishi wa Habari wakati akitoa taarifa ya Utendaji kazi wa Taasisi hiyo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2022 huku lengo la Wahudumu hao wa Afya kufanya Usajili hewa ikiwa ni kujipatia kipato kupitia malipo ya shirika linalosaidia kutoa Elimu ya Afya Nchini.

Ambapo alisema Takukuru kupitia vyanzo vya siri ilibaini kuwa watoa huduma za afya wanaohusika na kusajili watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi,wamekuwa wakifanya udanganyifu kwa kuwaingiza majina hewa ili kuonesha takwimu za wanaoishi na VVU kuonekana zipo juu kwa maslahi yao binafsi.

Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Tanga alibainisha kuwa katika ufuatiliaji wa TAKUKURU Mkoa ulibaini kuwa wahudumu wa Afya wanaohusika na zoezi la kuwasajili na kuwafuatilia wagonjwa wanaoishi na VVU wamekuwa wakilipwa posho ya gharama ya usafiri kupitia akaunti za Simu za mawasiliano kiasi cha sh 20,000 kwa siku kila wanapotoka kwenda kuwatembelea wagonjwa hao.

Alisema fedha hizo Hulipwa na Shirika la Afya la AMREF Tanzania kwa kazi ya kufuatilia kila Mgonjwa kwa lengo la kuhakikisha hali yake kiafya inaimarika kwa maana ya kutumia dawa kwa wakati na huduma nyengine zinazostahili.

Aidha alisema fedha hizo kulipwa moja kwa moja kwa mhudumu husika kupitia namba yake ya simu ya mkononi na ndiyo sababu inavyopelekea watumishi wasio waadilifu kuweka takwimu hewa kwa lengo la kujiongezea posho.

Alieleza katika ufuatiliaji uliofanywa na Takukuru kwa baadhi ya Zahanati ilibainika kuwa ni kweli kuna wagonjwa ambao siyo halisi kwa maana ya upatikanaji wake na hivyo kufanya udhibiti kwa kuchukua hatua.

Alisema kwamba hatua walizoanza kuchukua ni kufikisha kikao cha pamoja kati yao na ofisi ya Mganga Mkuu wa wilaya na watendaji wake wote wanaohusika na kuwahudumia watu wanaoishi na VVU pamoja na AMREF

Katika kikao TAKUKURU iliwasilisha yaliyobainika katika ukaguzi wa kutembelea Jumla ya zahanatini 7 kati ya 16 zilizopo katika wilaya ya Muheza na kubaini tatizo hilo“Alisema.

Hata hivyo alisema kwamba katika kikao kazi hicho taasisi hiyo mkoani hapa ilimuagiza Mganga Mkuu wa wilaya ya Muheza kufanya uhakiki wa takwimu za wagonjwa wote wanaoishi na VVU na kutoa taarifa ya uhakiki.

Alisema baada ya agizo hilo ilibainika kuwepo kwa Jumla ya wagonjwa hewa 313 ambapo idadi hiyo iliondolewa kwenye mfumo.

Pia alisema wahusika katika usajili wa wagonjwa hao hewa wamepewa barua za kujieleza kwa kitendo cha usajili wagonjwa hewa huku Wizara ya Afya ikitoa maelekezo ya kufanyika uhakiki kwa wagonjwa wanaotumia dawa ambao sio halisi.

Hata hivyo Taasisi hiyo inaendelea kuwasihi watumishi wote wa Umma kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni,taratibu,sheria na kiongozi iliyopo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!