Na Mwandishi Wetu
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya taifa ya Somalia, mchezo wa hatua ya pili ya mchujo ya kuwania kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za ndani (CHAN) kwenye uwanja wa Banjamin Mkapa.
Mshambuliaji Mpya wa Azam FC Abdul Suleiman ‘Sopu’ aliwanyanyua watanzania mnamo dakika ya 47 kipindi cha pili akifunga bao kwa Kichwa akipokea ‘Krosi’ safi ya Mlinzi wa pembeni, Kibwana Shomari..
Kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza, Timu ya taifa ya Somalia walikuwa nyumbani Benjamin Mkapa, Kikanuni kutokana na sababu za kiusalama nyumbani kwao. Mchezo wa mkondo wa pili utachezwa Julai 30, 2022 ambapo Taifa Stars itakuwa nyumbani kwenye uwanja huo huo wa Mkapa.
Taifa Stars inatakiwa kupata sare yoyote au ushindi ili kusonga mbele kwenye hatua inayofuata ili kujihakikishia nafasi nzuri ya kufuzu Michuano hiyo ya CHAN.
Mshindi wa jumla wa mchezo huo kati ya Taifa Stars dhidi ya Somalia atacheza na timu ya taifa ya Uganda (The Cranes) ambao utakuwa mchujo wa mwisho ‘Play Off’ ya kuwania kufuzu Michuano ya CHAN ambayo itafanyika nchini Algeria, kuanzia Januari hadi Februari, 2023