Taasisi za kifedha nchini zimehimizwa kuisaidia Serikali kukusanya na kutunza taarifa za Wamiliki Manufaa wa Kampuni kwa kuwa wanazitambua kampuni hizo kupitia huduma mbalimbali za kifedha wanazozitoa hapa nchini nia ikiwa ni kufichua maovu yanayofanyika nyuma ya Kampuni.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe Edward Mpogolo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika ufunguzi wa warsha ya utoaji elimu kwa taasisi za fedha juu ya dhana ya umiliki manufaa iliyofanyika leo tarehe 27 Juni, 2023 katika Kituo cha mikutano ya kimataifa cha Julius Nyerere(JNICC), jijini Dar es Salaam.
“Changamoto za taarifa za wamiliki ni kwamba watu wengi walikuwa wanatumia Kampuni kukwepa kodi, kupitisha fedha haramu, ugaidi na Serikali imeona iwe na uhakika wa kupata taarifa za wenye Kampuni hivyo kuwa na ulazima wa kukutana na taasisi za fedha”, amesema Mhe Mpogolo.
Mhe. Mpogolo amesema jitihada za Serikali haziwezi kufanikiwa bila taasisi za fedha, kwa kuwa ni watu muhimu sana, BRELA ni kiungo kati ya maelekezo, maagizo na sheria mbambali za Serikali lakini mtekelezaji wa sheria hii ni taasisi za fedha na ili kufanikiwa, Serikali inawahitaji kushirikiana ili kutimiza utekelezaji wa sheria iliyopitishwa.
Nae, Bw Andrew Mkapa, Mkurugenzi wa Leseni akimuwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA amesema kuwa Taasisi hushirikiana kwa karibu na taasisi za fedha katika utendaji kazi wa kila siku na ni matarajio ya BRELA kuwa warsha juu ya dhana ya Umiliki Manufaa itapata ushirikiano utakaozalisha ufanisi, kuibua michango mizuri yenye kujenga na kuwa na uelewa wa pamoja kwa manufaa ya wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kwa ujumla.
Bw. Mkapa ameongeza kwa kusema, BRELA pia imeona umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kwa taasisi za fedha kutokana na mabadiliko ya Sheria ya fedha ya mwaka 2020 iliyopitisha marekebisho ya Sheria ya Makampuni sura 212 na kanuni zake kupitishwa na Waziri mwenye dhamana na biashara nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji kutoka Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) Bi Tusekelege Mwaikasu amesema kuwa warsha hiyo imekuwa ya umuhimu kwao kwasababu ni sheria ambayo imewekwa kama muongozo na jukumu lao ni kutekeleza kwa kutoa taarifa zenye mashaka au matendo tofauti ya mtumiaji wa akaunti na kuwasaidia kujua mmiliki halali wa Kampuni husika iliyofungua akaunti kwenye benki hiyo.
BRELA imeratibu warsha ya siku mbili kwa taasisi za fedha ili kuwajengea uwelewa juu ya dhana ya Mmiliki Manufaa wa Kampuni ambapo mmiliki anatambulika moja kwa moja au kwa kupitia mtu mwingine mwenye zaidi ya asilimia tano (5%) ya uwekezaji au ufanyaji maamuzi kwenye Kampuni.