Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Ndugu Stephen Wasira, akizungumza kwa kutoa shukrani kwa kuaminiwa na kuchaguliwa katika nafasi hiyo mbele ya Viongozi na Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM unaofanyika katika ukumbi wa JKCC, Jijini Dodoma.
“Kazi yetu ya kwanza ni kushika dola kwa serikali zote Tanzania Bara na Zanzibar. Katika serikali za mitaa tayari tumefanya vizuri; sasa kazi tuliyonayo ni kukamata dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Tujiandae vema, na ikifika mwezi Oktoba tutakamata dola kwa kura nyingi za ushindi. Kura unazipata kwa kutekeleza ahadi na ilani ya chama chako. Sisi CCM tumetekeleza kwa kishindo chini ya Mwenyekiti na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“CCM hatuna sababu ya kushindwa uchaguzi. Miradi yote inatekelezwa kwa wakati na maendeleo yanafanyika.
“Twendeni tukashinde uchaguzi. Sababu tunazo, nia ipo, na uwezo tunao. Huu ndio wito wangu, na kazi inaanza.
“Nataka dunia ijue, wana CCM na wasio wana CCM, chama chetu ni cha umoja, amani, na maendeleo. Tunapewa nchi ili kufanya kazi, na kazi haiwezi kufanyika bila amani. Mwenyekiti wetu ana falsafa ya 4R, na mimi nasema kazi nitakayoanza nayo ni kuendeleza maridhiano. Wengine wanasema hakuna maridhiano. Hapana! Haturidhiani na mtu mmoja bali tunaridhiana na jamii yenye wadau wengi, pamoja na viongozi wa kidini. Tutasaidiana nao katika maridhiano kwa sababu CCM ni chama cha amani. Kama una chama chako kinachotaka vita, sisi tutazungumza na wewe kuwa huko hatuendi, kwa kuwa amani ni msingi wa maendeleo.”