Na Shomari Binda-Musoma
MASHUJAA wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) wametakiwa kuongeza ubunifu zaidi wanapofikisha ujumbe kwa jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Mara Dominicus Lusasi alipokuwa akifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Taifa wa SMAUJATA Sospeter Bulugu alipotembelea ofisini kwake.
Amesema anatambua kazi nzuri inayofanywa na mashujaa wa SMAUJATA lakini wanapaswa kuongeza zaidi ubunifu wanapokwenda kwenye jamii kutoa ujumbe ili kuiweka jamii sawa kuachana na masuala yasiyofaa yakiwemo ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia hivyo bila ubunifu katika mazungumzo uelewa inakuwa ni kazi.
Lusasi amesema licha ya kuzungumzia masuala ya ukatili yapo mambo mengine ambayo mashujaa wanaweza kuyazungumzia, Mara kuna mambo mengi likiwemo ziwa victoria ambapo kumekuwepo na uchafuzi ambao mashujaa wanaweza kuuzungumzia
“Mashujaa SMAUJATA wanapaswa kuwa wabunifu mnapokuwa mnatekeleza majukumu yenu ili jamii iweze kuwaelewa zaidi.
“Ofisi ya mkuu wa mkoa kupitia maendeleo ya jamii itaendelea kutoa ushirikiano kwa mashujaa wa SMAUJATA katika kampeni mnazozifanya za kupambana na ukatili wa kijinsia“, amesema
Mwenyekiti SMAUJATA Taifa Sospeter Bulugu amesema ushirikiano uliopo ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara ni mkubwa na maeneo mengine yanapaswa kuiga.
Amesema ziara yake mkoa wa Mara amejifunza mambo mengi ambayo atakwenda kuyafanyia kazi katika kupelekea ufanisi wa kazi.
Bulugu amesema kwa kuwa SMAUJATA tayari wamepata usajili rasmi zipo changamoto ambazo zitakwenda kumalizika.