Serikali imetoa rai kwa vijana nchini kufanya juhudi za kujikinga na maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI (VVU) pamoja na walio shuleni kuhakikisha wanazingatia masomo na kujiepusha na tabia hatarishi zitakazosababisha kupata maambukizi na kushindwa kuyafikia malengo yao.
Rai hiyo ilitolewa Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ugawaji Vishikwambi kwa walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kupitia mradi wa Timiza Malengo.
Mhe. Simbachawene alisema lengo la mradi huo ni kusaidia vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 kutimiza ndoto zao pamoja na kuwasaidia vijana walio ndani na nje ya shule kwa kuwajengea uwezo wa fikra , maarifa na maadili ili wawe salama dhidi ya maambukizi ya VVU.
“Kama Taifa tuna kila sababu ya kulinda kundi la vijana kuimarisha nguvu kazi ya Taifa , kukuza uchumi pia kujenga Taifa imara na lenye nguvu . Nia ya Serikali ni kuhakikisha tunakuwa na vijana wazalendo wanaotambua mchango wao katika jamii , wenye kujitolea katika shughuli za maendeleo ,” alisema Mhe. Simbachawene .
Pia aliongeza kuwa mradi huo unaogharimu takribani bilioni 55 unafadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa UKIMWI , Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) wasichana balehe na wanawake vijana wapatao 1,000,000,000 watafikiwa na mradi huo.
“Niwapongeze wadau wa maendeleo kwa kutambua umuhimu wa mapambano haya na udhibiti wa maambukizi ya VVU hususani kwa vijana na ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan inaridhishwa na utekelezaji wa mradi kwani umefanikiwa kutoka mikoa mitatu hadi mitano na Halmashauri 10 hadi 18 nchini,”aliongeza.
Aidha aliwataka Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zinazotekeleza mradi kusimamia kwa ufanisi pamoja na kuanisha Klabu za UKIMWI shuleni, kusimamia na kufuatilia uwajibikaji wa Maafisa Ugani katika usimamizi wa maendeleo ya utekelezaji wa mradi kwa walengwa na kusimamia matumizi sahihi ya zana kwa uendelevu wa mradi katika Halmashauri husika.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda alibainisha kwamba kukithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia shuleni na katika maeneo mbalimbali huchangia kwa kiasi kikubwa maambukizi mapya ya UKIMWI na afya za watoto na vijana kuathirika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dk. Leonard Maboko alieleza kuwa ni kusudi la tume hiyo chini ya mradi wa Timiza Malengo kuwezesha wasichana balehe na wanawake vijana kukaa shuleni kutimiza malengo yao na walio nje ya shule kupatiwa elimu ya ujasiriamali na kupewa ruzuku kuanzisha miradi midogo midogo kujikwamua kiuchumi