Theophilida Felician Kagera.
Shirika la wanaume wanaopitia changamoto mbalimbali kwenye maisha ya ndoa limetoa wito kwa wanaume Mkoa Kagera wajitokeze wazi kuziripoti changamoto za ukatili ili waweze kusaidiwa.
Ameyasema hayo Mwenyekiti wa SHIWACHANDO Mkoa Kagera Richard Leonard Mshashu wakati akizungumza na Blog hii ya Mzawa katika ofisi ya shirika hilo iliyopo kata ya Rwamishenye Manispaa ya Bukoba.
Richard awali ameanza kuelezea hali ilivyo kwa jamii juu ya vitendo vya ukatili kwa wanaume na wanawake vimekuwa vingi kutokana na sababu tofauti tofauti ambazo zimepelekea kuwepo kwa matukio mara kadhaa yenye kujaa ukatili wa ajabu.
Amefafanua kuwa tangu shirika hilo kufika Kagera mwaka 2022 limewapokea wanaume waliojitokeza na kuyaripoti matukio ya ukatili kwenye ndo zao ambapo takwimu zimekuwa zikiongezeka za wanaume wanamna hiyo.
Mwaka 2022 walijitokeza jumla ya wanaume 40,850 na kati ya hao 1,603 walipatiwa ushauri na kupata nafuu nakuweza kuendelea na maisha ya ndoa zao.
Amesema vitendo vya kikatili vimewasababishia madhara kadhaa wanaume hadi kutoweka majumbani mwao, kukwama kimaendeleo, kujinyonga kutoka na msongo wa mawazo wakati mwingine kuchukua hatua ya maamzi magumu kwa wenza wao hadi vifo.
Mwaka 2023 idadi yawanaume walioripoti matukio iliongezeka kufikia idadi ya wanaume 6013 ushauri ulitolewa dhidi yao hivyo jumla ya wanaume 3432 wanaendelea vizuri.
“Kwa kweli, kesi tulizozipokea hapa baadhi ni za aibu mno kuzitaja mfano mmoja wa wathiriwa huko Muleba alifanyiwa ukatili na mkewe wakuwekewa kinyesi cha binadamu kwenye chakula (mboga) yakulia ugali, hata mimi hapa nimewahi kumwagiwa kinyesi usoni cha binadamu na mke wangu, kule Ngara mwanaume alipigwa na mke wake tukio liliripotiwa polisi, pia Biharamulo kuna mama alimchoma kisu mume wake, vile vile Muleba mke alimchoma na kitu chenye ncha kali mumewe utumbo ukatokezea nje, kunyimwa unyumba nayo imekuwa nishida kubwa, tunapigwa kwa matukio mengi mno ya vitendo kwenye ndoa zetu hivyo wanaume wenzangu muda ni sasa tujitokezeni tuyasema yanayotukuta vunjeni ukimya ili yafanyiwe utatuzi maisha yaendelee kwa amani na upendo” amesema Richard.
Amevitaja vyanzo ni pamoja na ongezeko la mmomonyoko wa maadili kwenye jamii, watu kuishiwa moyo wa huruma, kutokuheshimiana, malezi mabovu kwa watoto, ushirikiano hafifu kwenye utafutaji kipato katika ndoa, ugomvi uliopitiliza na mengine mengi.
Amedokeza kuwa wanaume waliojitokeza wengi wao wenye matukio yenye unafuu walipewa ushauri namna ya kusaidiwa na wenye matukio ya jinai waliwaelekeza kuyaripoti Polisi.
Ameeleza adhima ya Shirika hilo ambalo makao makuu yake ni Dar es salaam limejikita zaidi kuunganisha ndoa na jamii kwa ujumla zaidi likihimiza suala la maadili kwani ndicho kitovu cha mambo yote.
Baada ya SHIWACHANDO kujitokeza na kuyatatua masuala yanayozikabili ndoa hususani kwa wanaume, hadi sasa limewapata wanachama 9480 kwa Kagera wanaoona umuhimu wa uwepo wa shirika hilo.
Idadi kubwa ya wanaume wanaoripoti kufanyiwa ukatili ni wilaya ya Muleba.
Mbali na hayo ameitaja changamoto ya ukosefu wa bajeti ya kifedha yenye kuwawezesha viongozi kuwazungukia wananchi wilaya za Mkoa Kagera ili kuwafikia watu wengi katika kutoa elimu kwani hata usafiri ni shida hivyo ameiomba serikali, wadau mbalimbali ndani ya nchi na nje ya nchi kuwiwa na kuwashika mkono kwa hali na mali ili shirika liweze kuendeleza mapambano imara katika kuunganisha jamii ya kitanzania.
Amehimiza maadili yaendelee kusisitizwa maeneo yote iwe shuleni, nyumba za ibada, kazini, nk.
Hata hivyo ameishauri serikali kupitia Bunge tukufu iwekwe Sheria mahususi inayowabana watu wanaokiuka suala la maadili ili kusaidia kupunguza matukio ya hovyo kwenye jamii.
Richard amemshukuru Mwenyekiti wa shirika taifa Ernest Josephat Komba pamoja naye waziri wa maendeleo jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu Mhe Dkt Dorothy Gwajima kwa jinsi walivyomsaidia kuunganisha ndoa yake iliyokuwa imeyumba na kusambaratika kwakipindi cha miaka nane mke wake hakuwepo nyumbani baada ya kushauriwa na viongozi hao alirejea na maisha yanaendelea vizuri.
Amehitimisha akiwasisitiza wanaume katu wasisite kuripoti changamoto zinazo wakabili ili zitatuliewe kwani wengine wamekuwa wakishindwa kujitokeza kwa madai ya aibu hata yeye ni muhanga wa matukio mazito ya kikatili alipojitokeza na kuyaweka wazi alisaidiwa na SHIWACHANDO pamoja na waziri Gwajima.