Home Afya Shirika la Americares lamwaga vifaa vyenye thamani ya Tsh Milioni 234 Bugando

Shirika la Americares lamwaga vifaa vyenye thamani ya Tsh Milioni 234 Bugando

Na Sheila Katikula, Mwanza

Shirika la Americares limetoa vifaa tiba vya upasuaji wa ugonjwa wa fistula ya uzazi vyenye thamani ya sh Milioni 234.2 kwenye Hospitali ya Rufaa Kanda Bugando iliyopo mkoani Mwanza

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla kwenye hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi amesema vitasaidia kutoa huduma ya matibabu kwa akina mama wenye ugongwa wa fistula ya uzazi ili waweze kuzuia vifo vitokanavyo na tatizo hilo.

Makilagi amelipongeza Shirika hilo kwa kutoa vifaa hivyo kwenye hospitali ya Bugando kwani vitasaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi wenye tatizo hilo.

Hata hivyo ameutaka uongozi wa hospitali ya Rufaa ya Bugando kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa ili viweze kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kanda Bugando, Dk Fabiani Massaga amesema zaidi ya wanawake 300 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, wanaugua ugonjwa wa fistula na wametibiwa katika hospitali hiyo ambapo kwa mwaka 2022 waliopata tiba walikuwa wanawake 373 na kati yao, 207 walifanyiwa upasuaji huku 166 wakipata tiba ya viungo.

Amesema asilimia kubwa la wagonjwa wa fistula wametokea kwa Kanda ya Ziwa,kwenye mikoa ya Shinyanga na Geita imetajwa kuwa na wagonjwa wengi wa fistula ambapo wataalamu kutoka hospitali ya Kanda Bugando kupitia huduma ya tiba mkoba wamekuwa wakifika katika mikoa hiyo ili kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ili kuwasaidia akina mama wakati wa kujifungua na kuwaepusha na hatari ya kupata ugonjwa huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi Shirika la Americares, Nguke Mwakatunde amesema takribani wanawake elfu tatu huugua fistula kila mwaka hapa nchini ambapo wanaofika katika matibabu ni takribani wanawake elfu mbili huku wanawake elfu moja wakikosa huduma kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa elimu ya kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Vifaa hivi vitasaidia kuboresha huduma za upasuaji wa fistula ya uzazi hapa Bugando, lakini pia shirika la Americares kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya litaendelea kushiriki juhudi mbalimbali za kutokomeza fistula hadi kufikia mwaka 2030” amesema Mwakatunde huku akishauri Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kusogeza huduma za fistula karibu na wananchi hadi ngazi za hospitali za rufaa za mikoa.

Naye shujaa wa fistula ambaye anatibiwa na hospitali ya Bugando Christina Mussa kutoka mkoani Mwanza wamelishukru shirika la Americares kwa msaada wa vifaa hivyo na kueleza kuwa vitasaidia kuboresha huduma kwa wanawake wanaougua ugonjwa huo.

Kwa upande wake Muuguzi wa hospitali hiyo Yustina Nungulla amesema ugonjwa huo unaosababishwa na uchungu pingamizi wakati wa kujifungua na kupelekea changamoto mbalimbali kwa wanawake.

Nawaomba wananchi kuachana na tabia ya kuwanyanyapaa wagonjwa wenye tatizo na badala yake kuwasaidia wagonjwa ili waweze kupata matibabu kwa haraka kwani fistula inatibika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!