Home Kitaifa DKT. NDUMBARO AWEKA JIWE LA MSINGI JENGO JUMUISHI TAASISI ZA KISHERIA

DKT. NDUMBARO AWEKA JIWE LA MSINGI JENGO JUMUISHI TAASISI ZA KISHERIA

❖ Ujenzi kugharimu shilingi bilioni 3.8, kukamilika ndani ya miezi 18

❖ Yasogeza huduma za kisheria na utoaji haki karibu na wananchi

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (wa kwanza kushoto) akipata maelezo ya michoro ya ujenzi wa jengo jumuishi la taasisi za sheria kutoka kwa Msanifu Majengo wa TBA, Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri, Wencelaus Kizaba wakiwa eneo la ujenzi wa jengo hilo Buswelu wilayani Ilemela mkoani Mwanza
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi (wa tatu kushoto) na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (wa pili kushoto) wakijiandaa kukagua ujenzi wa jengo jumuishi la taasisi za sheria wakiwa eneo la ujenzi Buswelu wilayani Ilemela mkoani Mwanza

Na Mwandishi wetu, OWMS, Mwanza

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) ameweka jiwe la msingi kwenye jengo jumuishi la taasisi za kisheria linalojengwa eneo la Buswelu Wilayani Ilemela mkoani Mwanza ambapo jengo hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia watumishi 70 wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

Waziri Dkt. Ndumbaro amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo utasogeza huduma za kisheria na utoaji wa haki karibu na wananchi hivyo mwananchi atapata huduma za kisheria sehemu moja na huduma za ustawi wa jamii na msaada kisheria

Vile vile, ameongeza kuwa ujenzi huo utagharimu shilingi bilioni 3.8 na unatumia fedha za ndani ambazo ni kodi za wananchi na huu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ambayo inaitaka tasnia ya sheria nchini kuwapa wananchi haki ya kisheria kwa karibu, kwa haraka na kwa gharama nafuu

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akifurahi baada ya kuweka jiwe la msingi la jengo jumuishi la taasisi za sheria lililopo eneo la Buswelu wilayani Ilemela mkoani Mwanza. Kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Khatibu Kazungu, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi

Amesema kuwa Serikali itaendelea kujenga majengo jumuishi nchi nzima kwa kila mkoa ikiwa ni pamoja na kuweka miundombinu mbalimbali na kutumia mifumo ya TEHAMA katika kuhudumia wananchi kwa kuwa taasisi za kisheria ni taasisi za utoaji haki hivyo ni muhimu kuimarisha miundombinu husika

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Khatibu Mizungu amesema kuwa majengo jumuishi yameonesha faida ya kwa watumishi kwa kufanya kazi kwa pamoja na yanajenga mahusiano mazuri baina ya taasisi za kisheria

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amesema kuwa matumizi ya pamoja ya fedha yamefanyika kwa kutumia fedha za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na za Ofisi ya Mashtaka ya Taifa ambapo fedha za Ofisi ya Mashtaka ya Taifa zimetumika kununua kiwanja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inagharamia ujenzi wa jengo hilo

Mhe. Jaji Dkt. Feleshi amesema kuwa uwepo wa jengo jumuishi utawezesha huduma zinazotolewa kupatikana katika eneo moja kwa kuwa Ofisi hizi zinategemeana katika utoaji huduma za kisheria kwa wananchi na itapunguza gharama kwa wateja kwa kuwa watakuwa wanapata huduma mahali pamoja

Akizungumza kwa niaba ya Mshauri Elekezi wa ujenzi wa jengo hilo kutoka Wakala wa Majengo Tanzania, Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri, Msanifu Majengo Wencelaus Kizaba amesema kuwa hadi sasa mkandarasi wa jengo hilo, SUMA JKT tayari amelipwa shilingi 885,422,794.72 kati ya shilingi bilioni 3.8 na TBA ambaye ndiye mshauri elekezi amelipwa shilingi 32,468,435 na ujenzi umefikia kiwango cha asilimia 35% na ni wa muda wa miezi 18 ambapo hadi sasa imetumika miezi saba na mkataba umeingiwa tarehe 19 Aprili, 2022 na ujenzi unatakiwa kukamilika tarehe 25 Oktoba, 2023.

Amefafanua kuwa ujenzi umetoa ajira kwa watanzania, wanafunzi wamepata mafunzo kwa vitendo na ununuzi wa vifaa vya ujenzi unafanyika kwa kununua bidhaa kutoka soko la ndani hivyo Serikali inapata mapato

Akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, ndugu Hassan Masala amesema kuwa uongozi wa Mwanza uko tayari kuendelea kusimamia ujenzi huo ili kuona ufanisi wa miradi mikubwa ya Serikali na watashirikiana na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ili Serikali iweze kufikia malengo iliyojiwekea

Uwekaji huo wa jengo la msingi umehudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende, Mkurugenzi wa Mashtaka, Silyvester Mwakitalu, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo, Mkabidhi Wasii Mkuu wa RITA, Angela Anatory, Naibu Msajili Mkuu wa Mahakama Kuu – Mwanza, Chiganga Tebwa, menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali; viongozi wa ulinzi na usalama wa Wilaya ya Ilemela, viongozi wa Tarafa, kata, Mtaa na wananchi kwa ujumla.

Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akimkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (wa kwanza kushoto) alipowasili kuweka jiwe la msingi jengo jumuishi la taasisi za sheria lililopo eneo la Buswelu wilayani Ilemela mkoani Mwanza. Wa pili kushoto anayefurahi ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi
Picha ya muonekano wa jengo jumuishi la taasisi za sheria linalojengwa eneo la Buswelu wilayani Ilemela mkoani Mwanza kwa ajili ya matumizi ya watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ya Taif ana Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wa mkoa huo

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!