Home Kitaifa SERIKALI YAWAKARIBISHA WANANCHI KUWASILISHA CHANGAMOTO ZINAZOHUSIANA NA KODI

SERIKALI YAWAKARIBISHA WANANCHI KUWASILISHA CHANGAMOTO ZINAZOHUSIANA NA KODI

Na. Scola Malinga na Saidina Msangi, WF, Dar Es Salaam.

Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), imekaribisha wananchi wenye changamoto zinazohusiana na kodi kuwasilisha malalamiko katika Taasisi hiyo ili ziweze kushughulikiwa ndani ya siku 30.

Wito huo imetolewa na Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi Bw. Robert Manyama, alipokutana na Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa Hazina Ndogo, alipokuwa akiitambulisha Ofisi hiyo pamoja na malengo na wajukumu ya kuundwa kwa Taasisi hiyo huru ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (Tax Ombudsman Service of Tanzania TOST).

Bw. Robert Manyama alisema kuwa Taasisi hiyo imeanzishwa kama jukwaa huru la kutoa usuluhishi wa malalamiko na taarifa za kodi kwa kuzingatia haki na usawa kwa mlalamikaji na mlalamikiwa.

Alisema kuwa Taasisi hiyo imeundwa na Serikali ikiwa na lengo la kushughulikia malalamiko ya walipa kodi yanayotokana na taratibu huduma na maamuzi ya kiutawala, yanayotokea wakati wa usimamizi wa sheria za kodi unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

‘‘Taasisi ya TOST jukumu la kuainisha maeneo yenye matatizo katika usimamizi wa sheria za kodi na ambayo ni vyanzo vya malalamiko ya walipa kodi nchini na kutoa mapendekezo ya marekebisho kwa Waziri wa Fedha, alifafanua Bw. Manyama.

Alieleza kuwa TOST inalenga kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani na kuwezesha upatikanaji wa suluhu kwa haraka na kwa usawa dhidi ya malalamiko yatokanayo na usimamizi wa sheria za kodi.

Bw. Manyama alisema TOST pia ina lengo la kuongeza imani ya wananchi dhidi ya mfumo wa usimamizi na ukusanyaji kodi nchini na ulipaji wa kodi kwa hiari kwa kuhakikisha kwamba taratibu na huduma sitahiki za usimamizi wa kodi zinafuatwa bila unyanyasaji.

‘‘Mtu yeyote ambaye haridhishwi na utendaji katika maeneo hayo niliyotaja ya utoaji wa huduma, taratibu na maamuzi za Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), anaweza kuwasilisha lalamiko kwa Msuluhishi ndani ya siku 90 tangu kutokea ili liweze kufanyiwa kazi, usuluhishi wa malalamiko ya kodi kwa wakati utapunguza kwa kiasi kikubwa pingamizi za kodi na migogoro ambayo isiyo na ulazima wa kupelekwa mahakamani’’, alifafanua Bw. Manyama.

Alisema kwa mujibu wa sheria malalamiko ya mlipakodi yanayakiwa kushughulikiwa ndani ya siku 30 na kuwasilisha taarifa kwa Waziri wa Fedha ndani ya siku 14, hivyo amehimiza walipakodi kutoa taarifa zinazohitajika kwa haraka zinapohitajika ili kuepuka kuchelewesha mchakato wa kushughulikia malalamiko yao.

Aliongeza kuwa dhamira ya Taasisi hiyo ni kushughulikia malalamiko ya kodi kwa usawa na kwa ufanisi, kutatua malalamiko dhidi ya usimamizi wa sheria za kodi kwa njia ya majadiliano na upatanishi huku ikiharakisha utatuzi wa malalamiko kwa kutumia taratibu zisizo na gharama kubwa au kuhitaji mwanasheria jambo litakalojenga imani ya walipa kodi kwa mfumo wa usimamizi na ukusanyaji wa kodi nchini.

Naye Meneja wa Malalamiko na Usajili Bi. Naomi Mwaipola, alisema kuwa Taasisi hiyo inatoa huduma bure kwa wananchi na imejipanga kuwahudumia wananchi katika mikoa yote nchini na kutoa rai kwa wahariri hao kufikisha taarifa kwa umma.

‘‘Ninatazamia na ninawaamini kuwa ninyi ni wajumbe wazuri kwa haya mliyosikia na mtapeleka ujumbe kwa Watanzania watakaokuwa wanahitaji huduma yetu na tunafika popote licha ya kuwa Makao Makuu yetu yapo Dodoma, ukiwa mkoa wowote unaruhusiwa kuleta changamoto yako na sisi tutakufikia,’’akisema Bi. Mwaipola.

Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) ilianzishwa mwaka 2019 kwa marekebisho yaliyofanywa katika sheria ya usimamizi wa kodi ya mwaka 2015 na inafanya kazi nchi nzima, na mifumo yake imeanza kujengwa mwaka 2023 ambapo imeanza rasmi kutoa huduma kwa wananchi.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!