Na. WAF – Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa tahadhari juu ya uwepo wa ugonjwa ambao bado haujajulikana mkoani Kagera katika Wilaya ya Bukoba Vijijini.
Taarifa hyo ameitoa leo Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu alipokuwa anaongea na waandishi wa Habari katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma.
“Ndugu Wananchi, Wizara imepokea taarifa za uwepo wa ugonjwa ambao bado haujajulikana mkoani Kagera katika wilaya ya Bukoba Vijijini, kata ya Maruku na Kanyangercko, vijiji vya Bulinda na Butayaibega.” amesema Prof. Nagu
Prof. Nagu amesema kwa mujibu wa taarifa hizi, jumla ya watu 7 wanasadikika walipata dalili za homa, kutapika, kutokwa damu maeneo mbalimbali ya mwili na figo kushindwa kufanya kazi.
Amesema kuwa watu watano kati yao wamefariki na wengine wawili wako hospitali wanaendelea na matibabu.
“Mwenendo wa ugonjwa huu unaashiria uwezekano kuwa ni ugonjwa wa kuambukiza hivyo Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu na kuchukua hatua za kudhibiti ili usisambae,” amesema Prof. Nagu
Aidha, Prof. Nagu amewataka wananchi kuwahi kituo cha kutolea huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu endapo ataona dalili kama kupatwa na homa, kutapika, kuharisha, kutoka damu na mwili kuishiwa nguvu.
Pia, amewakumbusha kuwahi Kutoa taarifa mapema kwenye kituo cha kutolea huduma kilicho karibu au kupiga simu namba 199 bila malipo endapo utamuona au kukutana na mtu mwenye dalili kama hizo.
“Mnatakiwa kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono ili kujikinga na magonjwa yote ya kuambukiza,” amesema Prof. Nagu.
Pia, amewataka wananchi Kushirikisha wataalamu wa afya katika shughuli za misiba na mazishi katika kipindi hiki, kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono.
Mwisho, amewakumbusha watumishi wa afa kuzingatia kanuni za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza (IPC) wakati wa kutoa huduma.