Na Ashrack Miraji Same Kilimanjaro
SERIKALI imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya kuanzwa kwa ujenzi wa majengo manne hospitali ya wilaya ya Jimbo la Same mashariki wilayani Same mkoani Kilimanjaro.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Anne Kilango Malecela wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi kwa viongozi wa mashina na matawi wa Chama cha Mapinduzi Tarafa ya Ndungu ambapo alisema kuwa hospitali hiyo ilikuwa hitajio kubwa kwa wnanachi ambao walikuwa wakitumia umbali mrefu kufuata huduma hospitali ya Same.
Alisema kuwa, serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo miradi ya sekta ya barabara, Elimu, Umwagiliaji, maji na Afya.
Mbunge huyo alisema kuwa, katika mwaka wa fedha 2024/2025 serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami katika barabara ya Ndungu mpaka Mkomazi kwa urefu wa kilomita 36.9
“Barabara hii ambayo itatusaidia kukuza uchumi wa sisi wananchi itakapokamilika uchumi utakuwa lakini pia nitumie nafasi hii niwaombe wananchi hasa vijana tumieni fursa hii kupata ajira lakini hakikisheni mnakuwa walinzi wa vifaa vitakavyoletwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii” Alisema Anne Kilango
Aidha Mbunge huyo alisema kuwa, serikali pia imeshatoa kiasi cha shilingi Bilioni 7 kwa ajili ya kuboresha skimu za umwagiliaji kata ya Ndungu na Kihurio ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi hao kwenda kwa wananchi na kusemea kazi zilizofanywa na serikali yao.
Pia Mbunge huyo ameahidi kuendelea kuwapambania wananchi wa jimbo hilo kwa kuwasemea ili serikali iweze kupeleka fedha kwa ajili ya kutatua matatizo ya wananchi pamoja na kupeleka miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Same, Abdillah Mnyambo alisema kuwa ndani ya Chama cha Mapinduzi kuna miiko na sifa za uongozi na kuwataka kuhakikisha wanawashawi wanachama wenye sifa za kuwa viongozi kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Aidha Mwenyekiti huyo aliwataka viongozi hao kutimiza wajibu waliopewa na Chama kwa vitendo.
“Chama cha Mapinduzi hakitafuti Wabunge wanaoenda kujionyesha Bungeni bali ni wale watakaoenda kuwasemea wananchi na kuwapigania kupata maendeleo na hili Mbunge Anne Kilango amelionyesha kwa vitendo hivyo niwaombe endeleeni kumsapoti kwa kumuunga mkono ili maendeleo ya jimbo la Same mashariki yasonge mbele” Alisema Mnyambo.