Ofisi ya Makamu wa Rais imefanya Kikao kazi cha kutambulisha Programu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuendeleza Mitaji kwa ajili ya Maendeleo (UNCDF) kupitia mfumo wa kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi (LoCAL).
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho leo Desemba 21, 2022 jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Mazingira Dkt. Andrew Komba amesema programu hiyo itaongezea jamii mtaji katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yana athari kubwa katika maisha yao ya kila siku.
Dkt. Komba aliyemwakilisha Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama amesema programu hiyo awamu ya kwanza ya utekelezaji ipo katika Halmashauri tatu za Chamwino, Kondoa na Mpwawa mkoani Dodoma ambapo baada ya kupata matokeo tarajiwa, itaendelea na kufikia hadi Halmashauri 10 hadi 15 katika awamu wa pili ya programu.
Amesema Halmashauri hizi zilichaguliwa kutokana na mpango tayari uliokuwepo wa DCF kupitia UNCDF walifanya kazi katika maeneo hayo na kiasi cha fedha kilichotolewa kinalenga katika kupanua shughuli ambazo tayari zinaendeela kutekelezwa.
Amesema kikao hicho ni fursa kwa washiriki kuweza kupitia taarifa mbalimbali za kimazingira zikiwemo biashara ya kaboni ambayo tayari Serikali imeandaa Mwongozo na Kanuni zake.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo pia, kikao hicho kitawapa fursa ya kujadili kuhusu Mchango wa kitaifa wa kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi (NDC), Tathmini ya athari ya Mazingira Kimkakati, Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira na taarifa ya masuala Jangwa yanayoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
“Huu ni mwendelezo wa jitihada za kitaifa za kushughulikia athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za binadamu hususan katika serikali ya mitaa, vijiji na vitongoji,” amefafanua.
Aidha, Dkt. Komba amesema nchi 24 duniani zinatekeleza programu hiyo huku Tanzania ikiwa mojawapo ambapo hukutanisha mawaziri wa kisekta wanaounda Bodi inayokutana kila mwaka kujadili namna ya kuwezesha jamii kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Serikali inaamini programu hii italeta tija iwapo itakuwa na ufanisi kwasababu ni miongoni mwa programu zinazotambua dhana ya kuona fedha za mabadiliko ya tabianchi zinamfikia mlengwa moja kwa moja kwa maana kijiji husika,” amesema.
Kikao hicho cha siku mbili kinahusisha washiriki kutoka katika Wizara mbalimbali ambazo zinashughulikia Mpango huu wa LoCAL chini ya washirika wa maendeleo UNCDF.