Na Englibert Kayombo WAF – Dar Es Salaam.
Kutokana na hali ya maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO-19 kuendelea kupungua hapa nchini na Dunian kote, Serikali imeondoa ulazima wa kuvaa barakoa isipokuwa pale inapobidi.
Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu leo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa UVIKO-19 katika Ofisi ndogo za Wizara zilizopo Jijini Dar Es Salaam.
“Kwa siku za hivi karibuni, idadi ya maambukizi mapya ya UVIKO-19 duniani yamekuwa yakipungua. Hali ya ugonjwa huu nchini pia imeonekana kupungua ikiwemo makali ya ugonjwa huu yanayopelekea watu kulazwa, uhitaji wa hewa tiba ya oksijeni, uhitaji wa mashine ya kusaidia kupumua na hata vifo” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Amesema sababu nyingine ilisababisha hali ya maambukizi kupungua kuwa ni uchanjaji wa chanjo ya UVIKO-19 ambapo kwa sasa asilimia 60 ya walengwa (wenye umri zaidi ya miaka 18) wamechanjwa.
Waziri Ummy amesema takwimu zinaonyesha kupungua kwa ugonjwa huo nchini Tanzania huku takwimu zikionyesha mpaka kufikia tarehe 7 Septemba 2022, Tanzania ilikuwa na jumla ya visa 35,747 vilivyothibitishwa kuwa vya maambukizi ya UVIKO-19 na vifo 808.
Amesema uchambuzi wa takwimu katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii na vituo vya kutolea huduma za Afya kwa tarehe 7 Septemba, 2022 unaonesha kuwa, kati ya watu 289 waliopimwa, watu 23 wamethibitika kuwa na maambukizi ya UVIKO-19.
“Kwa kuwa hali ya maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO-19 yanaendelea kupungua duniani kote na hapa nchini, Serikali inaondoa ulazima wa kuvaa barakoa isipokuwa pale inapobidi, mfano kwa wale wenye magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa na kwenye mikusanyiko ya ndani pale inapobidi” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema hatua nyinginezo ambazo zimelegezwa mara baada maambukizi ua ugonjwa huo kupungua kuwa ni; Kusitisha kufanya kipimo cha haraka (Rapid Test) kwa wasafiri wanaoingia nchini kutoka nchi zote wenye vyeti vya chanjo ya UVIKO- 19 au cheti cha RT – PCR; Kuongeza umri wa watoto kutoka nje ya nchi wanaotakiwa kusamehewa kupima UVIKO-19 kabla hawajaingia nchini kutoka umri wa miaka 5 (iliyokuwa awali) hadi miaka 12; magari ya abiria yanayoingia nchini kwa waliopata chanjo ya UVIKO – 19 pamoja na kusitisha matumizi ya vipimajoto (thermoscans) kuchunguza COVID-19 kwa wasafiri hao yamesitishwa.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imejipanga kuendelea kuelimisha na kuhamasisha wananchi kupata chanjo ya UVIKO-19 pamoja na kuendelea kufanya uchunguzi wa afya dhidi ya magonjwa ya milipuko kwa wasafiri wa kimataifa katika viwanja vya ndege vya kimataifa, bandari na mipaka ya nchi kavu.
“Wananchi waendelee kuzingatia unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi kwani afua hii ni miongoni mwa kanuni muhimu za afya katika kupunguza magonjwa ya kuambukiza” amehimiza Waziri Ummy Mwalimu.
Hata hivyo Waziri Ummy Mwalimu amewataka wananchi kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19 ili kuwa na kinga kamili ya kupambana dhidi ya ugonjwa huo.
Mwisho.