Na Shomari Binda-Musoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imekubali ombi la mbunge wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo kupandisha chuo cha ufundi Veta Musoma.
Ombi la mbunge Mathayo alilitoa bungeni alipouliza swali ni lini Waziri wa Wizara hiyo angefika Musoma na kukitembelea chuo hicho kwaajili ya kukiona chuo hicho na kuona uhitaji wake ili kukipandisha hadhi.
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Juma Omary Kipanga kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Profesa Adolf Mkenda leo septemba 26 amekitembelea chuo hicho.
Akizungumza chuoni hapo Naibu Waziri huyo amesema wametekeleza ombi la mbunge Mathayo ya kufika chuoni hapo na kupata taarifa juu ya chuo hicho.
Amesema taarifa imeeleza mahitaji yanayohitajika kuwepo chuoni hapo ili kukipandisha hadhi na kutoa maelekezo ili yaweze kutekelezwa.
Kipanga amesema moja ya mahitaji ni kuongezwa kwa kozi kutoka 9 na kufikia 10 pamoja na kuongezwa kwa madarasa,mabweni,eneo la kupata chakula,jiko pamoja na kalakana.
Naibu Waziri huyo amesema wizarani kuna fedha na kumuagiza mkuu wa chuo cha Veta Musoma na mkurugenzi wa Veta kanda ya ziwa kuandaa barua za maombi ya mahitaji hayo na kuziwasilisha.
” Nimefika chuoni hapa leo kwa niaba ya Waziri na Katibu Mkuu kufuatia swali lililoulizwa bungeni na mheshimiwa Mathayo ya kuomba Waziri afike.
Mbunge ni mfatiliaji licha ya kuuliza bungeni amekuwa mfatiliaji na leo Wizara imefika tumeona na kutoa maelekezo na maombi yanakwenda kutekelezwa”,amesema.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo amemshukuru Naibu Waziri huyo kwa kufika chuoni hapo kwa niaba ya Waziri kama slivyoomba bungeni.
Amesema chuo hicho kikipandishwa hadhi kitatoa fursa zaidi kwa vijana wa Musoma mjini na Tanzania kupata mafunzo zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka amesema mji wa Musoma utachangamka kama kutakuwepo na vyuo vingi vikubwa vitakavyo kusanya wanachuo wengi