Home Kitaifa SERIKALI YAJIZATITI KUTATUA CHANGAMOTO YA KUKOSEKANA UMEME VIJIJINI

SERIKALI YAJIZATITI KUTATUA CHANGAMOTO YA KUKOSEKANA UMEME VIJIJINI

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali ya Awamu ya Sita, imejizatiti kuhakikisha inaondoa changamoto ya umeme hapa nchini, kuanzia kwenye vijiji, kata, wilaya na mikoa.

Mhe. Kapinga amesema hayo leo Oktoba 10, 2023 wakati wa hafla ya uwashaji umeme kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vijiji Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika zahanati ya Lundumato iliyopo kijiji cha Ukata, wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma.

“Serikali ya Awamu ya Sita, imejizatiti katika kuhakikisha tunaondoa changamoto ya umeme hapa Ukata, jimbo lote la Mbinga Vijijini lakini kwa wilaya yote ya Mbinga na mkoa wote wa Ruvuma. Kwa hapa Ukata, kati ya vijiji vinne vya Litoho, Liwanga, Ukata na Ulima, vijiji vitatu vimeshapata umeme.

Ameendelea kusema kuwa, wao kama Wizara hawatawaangusha Wananchi wa Ukata, na hata hakikisha kijiji kilichobaki nacho kinapata umeme kabla mwaka haujaisha.

“Maendeleo ni hatua ndugu zangu, mradi huu ambao tunaufanya, vijiji vyote vitapata umeme. Hatutapindua huu mwaka bila kijiji kupata umeme, kama kuna kijiji chochote ambacho hakijapata umeme, tutahakikisha kinapata umeme kabla hatujapindua huu mwaka 2023. Tunapoanza 2024 tunaanza kupeleka umeme kwenye vitongoji,” amesema Mhe. Kapinga.

Kwa upande wake Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Evance Kabingo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili katika Kata ya Ukata amesema, “Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga kiasi cha shilingi bilioni 1.19 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa usambazaji wa umeme katika vijiji vinne vya Ukata, vijiji vitatu vimeshafikiwa na miundombinu ya umeme na kijiji kimoja kazi bado inaendelea”.

Amesema gharama ya uwekaji miundombinu ya umeme katika kijiji cha Ukata utagharimu shilingi milioni 128.46 katika kijiji cha Ulima ambacho kazi inaendelea, itakapokamilika kazi hiyo, Serikali itakuwa imetoa shilingi milioni 269.

Aidha amesema kuwa, kazi ya uwekekaji miundombinu ya umeme katika vijiji hivyo inaendelea ili kuhakikisha vijiji vyote vinne vinapata umeme.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!