Home Kitaifa SERIKALI KUPITIA TASAF YAJENGA BWENI KIJIJI CHA BUKUNDI KUONGEZA UFAULU WA WANAFUNZI...

SERIKALI KUPITIA TASAF YAJENGA BWENI KIJIJI CHA BUKUNDI KUONGEZA UFAULU WA WANAFUNZI NA KUWAEPUSHA NA MIMBA ZA UTOTONI

Sehemu ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bukundi wilayani Meatu wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule hiyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (Wapili kutoka kushoto) akizungumza jambo na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu (Wakwanza kushoto) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua iliyolenga kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule ya Sekondari Bukundi wilayani Meatu. Wakwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Meatu Mhe. Fauzia Ngatumbura.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (Wakwanza kulia) akisikiliza taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi shule ya Sekondari Bukundi wilayani Meatu, wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule ya Sekondari Bukundi wilayani humo. Katikati ni Mkuu wa Wilaya Meatu, Mhe. Fauzia Ngatumbura na wakwanza kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu Mhe. Prisca Kayombo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu akitoa salamu za TASAF wilayani Meatu, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) yenye lengo la kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule ya Sekondari Bukundi wilayani humo.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Bukundi wilayani Meatu wakimsikiliza Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule ya Sekondari Bukundi wilayani humo.
Mwonekano wa bweni la wanafunzi wa shule ya Sekondari Bukundi wilayani Meatu, linalojengwa kwa ufadhili wa TASAF.

Na. Veronica Mwafisi – Meatu

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imejenga bweni katika Shule ya Sekondari Bukundi iliyopo Kijiji cha Bukundi wilayani Meatu, ili kuweka mazingira rafiki ya kuongeza ufaulu wa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuwaepusha na changamoto ya mimba za utotoni.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo, mara baada ya kukagua bweni la wanafunzi wa shule ya Sekondari Bukundi akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.

Mhe. Ndejembi amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha hizo za TASAF na kujenga bweni hilo kwa ajili ya kutatua changamoto na adha zinazowakabili wanafunzi wa eneo hilo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu ili kuhudhuria masomo.

Kutokana na umuhimu wa bweni hilo, Mhe. Ndejembi ametoa mwenzi mmoja kwa viongozi na wasimamizi wa ujenzi wa bweni hilo kushirikiana kikamilifu na TASAF ili likamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma.

Bweni hili likikamilika kwa wakati litaongeza ufaulu na kusaidia kuondoa changamoto ya mimba za utotoni, kwani wanafunzi wataishi katika eneo hili la shule badala ya kwenda kuishi kwenye jamii ambayo ina changamoto nyingi,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, licha ya TASAF kuwezesha mradi wa bweni hilo lakini imejenga miradi ya maji, zahanati na vituo vya afya katika kipindi kifupi cha uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo amewataka wananchi wa Kijiji cha Bukundi kulinda miradi hiyo ili iwanufaishe wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani.

Sisi wananchi wa Bukundi tuna jukumu moja la kulinda miradi hii kwa manufaa yetu kwani serikali imetumia fedha nyingi kuitekeleza miradi hiyo,” Mhe. Ndejembi ameongeza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Fauzia Ngatumbura amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa bweni hilo la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Bukundi ambalo litaboresha mazingira ya wanafunzi kusoma.

Mhe. Fauzia amesema, shule ambayo bweni hilo limejengwa ipo katika jamii ya wafugaji ambao wanaishi maeneo ya mbali na shule hiyo, kutokana na umbali huo watoto wengi walitamani kusoma lakini walishindwa kutokana na kutembea umbali mrefu, hivyo bweni hilo litasaidia kuondoa changamoto hiyo.

Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu amewasisitiza wananchi wa Kijiji cha Bukundi kuilinda miundombinu ya bweni hilo kwani litawawezesha wanafunzi kupata elimu bora kwa ajili ya manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Bukundi wilayani Meatu, linalojengwa kwa ufadhili wa TASAF litakuwa na uwezo wa kuwahudumia wanafunzi 80.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!