Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa majisafi wa Makongolosi, Chunya mkoani Mbeya ambao umeboresha kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi wa eneo hilo na kusisitiza Serikali imejipanga kutoa huduma kwa wananchi wake.
Mhe. Samia akiongea na wakazi wa Chunya katika uwanja wa Shule ya Msingi Makongolosi, Kata ya Bwawani amesema serikali inatumia fedha nyingi ili wananchi wapate huduma bora ya maji ambapo mradi huo umewezesha kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 10 hadi asilimia 70.
“Serikali itaendelea kuhudumia wananchi kwa nguvu zote wapate huduma ya majisafi” Mhe. Samia amesema na kuongeza kuwa yeye kama mama anaelewa adha wanayopata akina mama inapotokea upungufu wa maji hivyo mradi huo umeondosha hali hiyo katika jamii.
Ameongeza kuwa mradi wa maji wa Makongolosi utazalisha maji kiasi cha lita milioni moja na nusu, zaidi ya mahitaji ya sasa ambayo ni lita milioni moja nukta mbili. Pamoja na hilo, Amesisitiza hali itazidi kuwa nzuri kwa sababu mkoa wa Mbeya una jumla ya miradi ya maji ipatayo 50.
Katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amesema kinachoendelea hivi sasa katika mradi huo ni pamoja na kuwaunganishia wananchi huduma ya maji katika makazi yao.