-Wafanyabiashara watakiwa kuchangamkia fursa, wachimbaji wadogo kuendelea kuwezeshwa vifaa
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ipo tayari kununua madini kutoka kwa wafanyabiashara wa madini nchini kwa bei ya soko la dunia ikiwa ni mkakati wa kuongeza mzunguko wa fedha, wafanyabiashara hao kupata faida zaidi na kuongeza Fedha za Kigeni Nchini.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Desemba 14, 2023 jijini Dodoma kwenye kikao chake na wadau wa madini ikiwa ni pamoja na wachimbaji wa madini, wachenjuaji wa madini, wafanyabiashara wa madini, watendaji wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania chenye lengo la kuangalia namna ya kuwawezesha wadau wa madini kwenye shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini hasa kwenye eneo la kuwawezesha kupata mikopo na kufanya biashara nchini na kupata faida huku Serikali ikipata kodi na kuongeza Fedha za Kigeni.
Akielezea mikakati ya kuwawezesha wadau wa madini nchini, Mhe. Mavunde amesema kuwa awali, Wizara ya Madini ilikaa na Taasisi za Kifedha kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu namna bora ya kuwawezesha wadau wa madini kupitia mikopo na kusisitiza kuwa mikakati mingine imeendelea kuwekwa ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia maeneo ya kuchimba madini pamoja na vifaa.
“Kumekuwepo na changamoto ya wafanyabiashara wa madini kutokuwa na mitaji ya uhakika hivyo kulazimika kuuza madini yao nje ya nchi kwa makubaliano maalum, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuja na mkakati wa kuwawezesha wafanyabiashara wa madini kwa kuuza madini yao nchini kulingana na bei ya soko la dunia, ni vyema mkachangamkia fursa hii ili kupata faida zaidi na Sekta ya Madini kuendelea kuchangia kwa kiwango kikubwa kwenye uingizaji wa fedha za kigeni,” amesema Mavunde.
Akielezea manufaa ya madini kuuzwa kwa Benki Kuu ya Tanzania, Waziri Mavunde amesema kuwa sambamba na wafanyabiashara kuuza madini yao kulingana na bei ya soko la dunia na kupata faida, kutakuwepo na ongezeko la fedha za kigeni na kuongezeka kwa mzunguko wa fedha nchini.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Taasisi nyingine itaendelea kutoa mafunzo kwa wachimbaji wa madini na wafanyabiashara wa madini ili shughuli zao ziwe na tija na kutimiza vision ya 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwapatia wachimbaji wadogo wa madini vifaa hususan mitambo ya uchorongaji miamba na kuongeza kuwa, malengo yamewekwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ifikapo Juni, 2024 tayari mitambo ya uchorongaji miamba 15 itakuwa imeshaletwa nchini.
Ameendelea kusisitiza kuwa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati imeweka mikakati ya kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana katika maeneo yote yenye shughuli za uchimbaji wa madini ili kuongeza uzalishaji na Serikali kupata kodi zaidi.
Wakati huohuo Waziri Mavunde amewataka wamiliki wote wa leseni za madini kuendeleza maeneo yao kama Sheria ya Madini na kanuni zake inavyowataka na kusisitiza kuwa hatua zitachukuliwa kwa wasioendeleza maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuwaandikia hati za makosa, kuzifuta na kuwapatia watu wengine wenye nia ya kuendeleza maeneo hayo.