Home Kitaifa SERIKALI INAZINGATIA HAKI ZOTE KWA WANAOHAMA KWA HIARI NGORONGORO

SERIKALI INAZINGATIA HAKI ZOTE KWA WANAOHAMA KWA HIARI NGORONGORO

Na Mwandishi Wetu.

Serikali imefafanua kuwa itaendelea kuzingatia utoaji wa haki zote kwa wananchi wanaoamua kwa hiari kuhama kutoka kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kupisha uhifadhi na kwenda kwenye maeneo wanayoyataka ikiwa ni pamoja na maeneo yaliyotengwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Murtalla Mbillu ametoa kauli hiyo alfajiri ya leo Aprili 7, 2024 makao makuu ya zamani ya Hifadhi ya Ngorongoro wakati alipokuwa akiwaaga jumla ya wananchi 422 kwenye walioamua kuondoka kwa hiari kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kupisha uhifadhi na kwenda kwenye maeneo waliyoyachagua.

Bila shaka mnatambua kuwa pamoja na Serikali kuwalipa fidia na motisha bado mkifika katika Kijiji cha Msomera mtapata huduma zote za msingi ikiwa ni pamoja na kupatiwa nyumba kwenye kiwanja cha ukubwa wa ekari 2.5 na ekari tano za kufanya shughuli za kilimo, eneo la malisho pamoja na huduma za elimu, afya, umeme na maji”. Amesisitiza Mbillu.

Amefafanua kuwa zoezi la kuhama ni zoezi la hiari ambapo mtu mwenyewe bila kushinikizwa na mtu ana hiari ya kuondoka lakini asitokee mtu wa kuwarubuni na kuwadanganya watu walioamua kuhama kwa hiari yao kwa kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wanafanya jinai na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Mwakilishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Msemaji wa Wizara hiyo, John Mapepele amewapongeza wananchi walioamua kwa hiari kuondoka kupisha uhifadhi huku akimshukuru rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa na dhamira ya kuboresha maisha ya wananchi.

Aidha, amesema dhamira ya Serikali ni kutaka wananchi wake wanapata haki zao za msingi za kuishi maisha bora na kupata huduma zote za kijamii kama elimu na afya bila kubughudhiwa na mtu.

Kaimu Kamishina wa Hifadhi ya Ngorongoro Victoria Shayo amewataka wananchi hao walioamua kuhama kwa hiari kuwa mabalozi wazuri kuwashawishi wananchi waliobaki kuchukua maamuzi sahihi ya kupisha uhifadhi.

Akitoa taarifa ya zoezi hilo Kaimu Meneja wa Mradi kuhamisha wananchi wa Hifadhi ya Ngorongoro, Flora Assey kaya 60 zenye watu 353 zimeelekea Kijiji cha Msomera wakati kaya 13 zenye watu 69 zimeelekea Meatu Simiyu na kaya zilizobaki zimeelekea simanjiro na Arusha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!