Home Kitaifa SERIKALI INA MAHUSIANO MAZURI NA SEKTA BINAFSI-MAJALIWA

SERIKALI INA MAHUSIANO MAZURI NA SEKTA BINAFSI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema maendeleo yaliyopo nchini hivi sasa yametokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya Serikali na sekta binafsi.

Maendeleo tunayoyaona nchini kwetu katika kila sekta yanategemea mchango wa Serikali pamoja na sekta binafsi. Dhamira na maono ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuimarisha sekta binafsi ili ihuishwe na kuwa mshindani katika kuleta maendeleo makubwa kwa nchi yetu,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumanne, Julai 23, 2024) wakati akizungumza na wadau wa sekta binafsi nchini kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sekta Binafsi Tanzania kwa mwaka 2024 yaliyofanyika Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam.

Wiki ya Sekta Binafsi Tanzania inaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 25 ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Amezitaka wizara na taasisi za Serikali ziendelee kupokea maoni ya sekta binafsi na kuhakikisha yanazingatiwa katika marekebisho ya sera na sheria za biashara ili kuondoa vikwazo vya urasimu na kuboresha taratibu za usajili na uendeshaji wa biashara nchini kwa kuwezesha upatikanaji wa vibali na leseni kwa haraka na kwa urahisi.

Pia amezitaka wizara zinazohusika na viwanda, biashara na uwekezaji zihakikishe zinabuni mbinu za kukuza na kusaidia biashara ndogo na za kati (SMEs). “Wekeni mazingira mazuri ya upatikanaji wa mikopo nafuu, mafunzo na ufikiaji wa masoko ili kusaidia biashara ndogo na za kati kukua na kuchangia katika uchumi. Biashara hizi ni sehemu muhimu ya kuimarisha sekta binafsi.

Akielezea jitihada ambazo zimechukuliwa ili kukuza sekta binafsi na uwekezaji, Waziri Mkuu amesema Serikali imeimarisha mazingira ya biashara kwa kufanya marekebisho katika sera na sheria za biashara ili kuondoa vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara na wawekezaji.

Hatua hizi zimejumuisha kuboresha taratibu za usajili wa biashara, kupunguza urasimu, na kuongeza uwazi, kutoa fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, nishati, miundombinu, utalii, viwanda na kuanzisha maeneo maalum ya uwekezaji.

Amesema Serikali imewekeza katika miundombinu ya usafirishaji, nishati, maji na mawasiliano ambayo ni muhimu kwa shughuli za uwekezaji na biashara. “Hatua hii inalenga kuimarisha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje,” amesema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzugumza na washiriki wa hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuasisi falsafa mpya ya kushirikiana na Sekta binafsi ikiwemo kuondoa ukiritimba wa mawazo.

Rais wetu yeye anaamini na anakiri katika dhana ya kusikiliza sauti na mawazo ya wengine ili kuweka mazingira bora ya mahusiano kati ya Sekta binafsi na Serikali”

Amesema kuwa kupitia falsafa hiyo imeshuhudiwa Rais Dkt. Samia akiendesha vikao vya kubadilishana mawazo mara kwa mara na makundi tofauti ya sekta binafsi yaliyojikita katika sekta mbalimbali kwa kusikiliza changamoto, kujifunza mafanikio na kutengeneza mfumo thabiti na sahihi wa kusonga mbele kwa manufaa ya pande zote mbili

Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema katika mwaka huu wa fedha, wizara hiyo imeweka vipaumbele sita ambavyo vinalenga kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Mweyekiti wa TPSF, Angelia Ngalula, alisema kuwa wanatamani kuona Tanzania inakuwa kitovu cha Afrika kutokana na rasilmali ilizonazo. “Pia tunatamani kuona biashara nyingi zinarasimishwa na wigo wa walipakodi unaongezwa,” alisema.

Alisema wakati TPSF inaanzishwa, ilikuwa na wanachama 33 lakini kwa sasa imefikisha wanachama zaidi ya 500 ambao wanajumuisha vyama vya wafanyabiashara na makampuni makubwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!