NA.MWADISHI WETU
Serikali imeendelea kuimarisha uratibu katika utekelezaji wa dhana ya Afya Moja kwa kushirikiana na wadau wote wa Afya na wadau wa maendeleo kwa ujumla ili kulinda afya ya jamii na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa mahala salama wakati wote dhidi ya matishio mbalimbali ya kiafya.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Bw. Prudence Constantine wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Viungo wa Afya Moja walipokutana kwa siku mbili kwa lengo la Kufanya Tathimini ya Utekelezaji wa Shughuli za Afya Moja kwa mwaka 2022 tarehe 13 Disemba, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Edema Mkoani Morogoro.
Alisema kuwa, Serikali imeendelea kuimarisha uratibu katika utekelezaji wa shughuli za Afya Moja kwa kutekeleza masuala kadhaa ikiwemo kufuta Dawati la Afya Moja na kuanzisha Sehemu ya Afya Moja (One Health Section) katika Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na kuhuisha Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja 2015 – 2020 kwa kushirikiana na wadau.
Akieleza kuhusu dhana ya Afya Moja alisema,inawakutanisha wataalam na wadau kutoka sekta mbalimbali, hususani sekta za Afya ya Binadamu, Mifugo, Wanyama pori, Mazingira na Kilimo katika kutekeleza Agenda ya Usalama wa Afya Duniani.
“Dhana hii ina manufaa makubwa hasa katika nchi zinazoendelea kwa kuwa inatumia rasilimali chache zilizopo kwa ufanisi weye matokeo chanya,” alisisitiza.
Alifafanua kuwa ushirikiano baina ya wataalam na sekta za Afya ya Binadamu, Wanyama, Kilimo na Mazingira (Afya Moja) hivi sasa ni agenda ya dunia ambapo imedhihirika kupunguza gharama katika kushughulikia tishio la milipuko ya magonjwa yanayotokana na vimelea vinavyoweza kuenea kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu katika mazingira mbalimbali.
Pia ushirikiano baina ya sekta zote za Afya Moja unategemea sana maafisa viungo waliopo katika sekta hizo ili kusaidia utendaji kazi wa Sehemu ya Afya Moja.
“Tuendelee kutekeleza majukumu yetu ipasavyo kama maaafisa viungo ili sekta zetu zishiriki kikamilifu katika utekelezaji wa dhana ya afya moja na kuleta matokeo chanya katika kupanua na kuimarisha ushirikiano baina ya sekta/taaluma mbalimbali katika hatua zote za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na hatari nyingine za afya zinazohitaji ushiriki wa sekta zaidi ya moja na taaluma mbalimbali,”alieleza Prudence
Aidha ushirikiano huu pamoja na wadau wengine ikiwemo jamii, kimsingi unaongozwa na sekta/wizara za msingi (lead Ministries) ambazo ni Afya ya Binadamu, Wanyama (Mifugo na Wanyama Pori), Mazingira na Kilimo katika ngazi zote.
“Ni imani yangu kuwa, mnatambua umuhimu wa kuimarisha na kuboresha utekelezaji wa dhana ya Afya Moja nchini na hatimaye kulinda na kuboresha afya ya binadamu, wanyama na uhifadhi wa mazingira pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchini,”alisema Prudence.
Aidha ushirikiano huu pamoja na wadau wengine ikiwemo jamii, kimsingi unaongozwa na sekta/wizara za msingi (lead Ministries) ambazo ni Afya ya Binadamu, Wanyama (Mifugo na Wanyama Pori), Mazingira na Kilimo katika ngazi zote.
“Ni imani yangu kuwa, mnatambua umuhimu wa kuimarisha na kuboresha utekelezaji wa dhana ya Afya Moja nchini na hatimaye kulinda na kuboresha afya ya binadamu, wanyama na uhifadhi wa mazingira pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchini,”alisema Prudence.
AWALI
Afya Moja ni dhana ya kimataifa iliyoridhiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (OIE), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Programu ya Kimataifa ya Mazingira (UNEP) kupitia “Global Health Security Agenda” (GHSA) na wadau wengine wa Afya duniani kote.
Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (OIE) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) yamekuwa yakishirikiana duniani kote na kutoa wito kwa wataalamu wa sekta za Afya ya Binadamu, Wanyama na Mazingira kuongeza na kuimarisha ushirikiano na mawasiliano ili kuboresha ufanisi katika kukabiliana na tishio la magonjwa ya kuambukiza yanayoenea kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na yanayovuka mipaka; tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, usalama wa chakula na lishe, afya ya mazingira, usalama na ulinzi wa vimelea hatarishi vya magonjwa na changamoto zingine zinazokabili afya ya jamii zinazohitaji nguvu ya pamoja.
=MWISHO=