Serikali imedhamiria kufufua kilimo cha mazao ya Biashara katika vijiji vitatu vya kata ya Nongwe wilaya ya Gairo mkoani Morogoro kwa kuanza na Kilimo cha Karafuu na Parachichi, ambapo kwa miaka mingi wakazi hao wameshindwa kunufaika, ikisababishwa na ubovu wa miundombinu hasa barabara kuyafikia masoko.
Akizungumza na wakazi wa Kata hiyo yenye vijiji vitatu, miongoni mwa maeneo yaliyobarikiwa kuwa na ardhi yenye Rutba, Joghrafia yake eneo kubwa ni Milima na mabonde makubwa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema Changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara imekuwa ikikwamisha shughuli za kilimo hasa kwa mazao ya biashara na kusalia kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Mkoa huyo amewagiza wakala wa barabara Tanzania TANROSDS na Wakala wa barabara mijni na vijijini TARURA kufanya ukarabati wa miundombimu ya barabara ya Nongwe ili wakulima waweze kusafirisha mazao yao kufikia soko la ndani njee ya nchi.
Tayari Kumekwisha fanyika uhamasishaji kwa wakazi wa kata hiyo kujikita kwenye uzalishaji kilimo cha mazao ya Biashara na tayari mwitikio ni mkubwa, wakisema kwa miaka yote kilicho wakwamisha ni kutowekea mkazo na ubovu wa miundombinu ya barabara unasababisha kutofikia masoko.
Mpango uliopo ni kuwa na wakulima wa mfano wakianza na kikundi cha wakulima wa Parachichi 42 waliowezeshwa mbegu na vitendea kazi, pia kuanzisha kitalu na kuotesha Miche 30,000 ya Karafuu kwa mwaka wa kwanza, ikisisitizwa idara ya kilimo kufuatilia kwa karibu suala hilo.