Na Neema Kandoro Mwanza
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Slaa amesema serikali haitalipa fidia kwa watu wanaovamia ardhi hivyo akazitaka halmashauri zote nchini kuweka alama na kutoa elimu kwa wananchi kuepuka adha hiyo.
Slaa alibainisha hayo Jijini Mwanza alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali ziarani kuelezea mpango wa serikali kufikia vijiji 975 kutatua migogoro na kuondoa changamoto ya ujenzi wa kiwanja cha ndege Mwanza.
Alisema watu waliovamia uwanja wa ndege na kujenga nyumba hawawezi kulipwa kwani eneo hilo lilikuwa limetengwa muda mrefu kwa matumizi hayo.
Slaa aliwataka watumishi wa ardhi kote hapa nchini kuweka alama kwa maeneo yaliyotengwa na kutoa elimu kwa watu juu ya matumizi ya ardhi ili kuondokana na changamoto ya uvamizi wa ardhi unaosababisha ugomvi kwenye jamii.
Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoani Mwanza Happiness Mtutwa alisema kuwa wananchi wote wahakikishe kuwa wanapima ardhi yao na kupata hati miliki ili kuondoa usumbufu usio wa lazima.
Vilevile aliwataka wananchi kutokuendeleza ardhi bila ya kupata ridhaa toka kwenye idara yao kwani kwa sasa waneboresha utendaji kazi zao.