Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ametatua mgogoro uliodumu kwa muda mrefu wilayani Karatu baada kuagiza bei ya maji iwe shs 1,300 kwa unit.
Pia, ameelekeza kuwepo kwa chombo kimoja kitakachosimamia utoaji wa huduma ya maji katika mji huo na bei iwe sh1,300 kwa uniti1 badala ya sh 3,000
Waziri Aweso ameagiza pia kuungana kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Karatu (KARUWASA) na Mamlaka ya Utoaji wa Huduma ya Maji Vijijini (KAVIWASU) na kutengeneza chombo kimoja ambacho kitatoa huduma kwa wananchi.
Pamoja na mabadiliko hayo, Waziri Aweso amesema Serikali itatoa shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji wa wilaya hiyo na kuagiza mamlaka husika zianze kutangaza zabuni ya mkandarasi atakayetekeleza mradi wa kusambaza maji.
Amesema hayo baada ya kusikiliza maoni ya wananchi na wadau mbalimbali wa maji wilayani humo ambapo awali kulikuwa na mgawanyiko wa maslahi ikiwemo Kaviwasu kutoza uniti moja kwa sh. 3000 huku Karuwasa ikitoza sh,1,750 kwa bei za majumbani.
Waziri Aweso amesema uwepo huo wa chombo kimoja utawezesha maslahi ya wananchi ikiwemo utoaji wa huduma bora za maji pamoja na kuhakikisha miundombinu ya maji haiharibiki.
Amesisitiza kuwa hakuna mtumishi yoyote atakayefukuzwa baada ya kuungana Karuwasa na Kaviwasa kwa kuwa watakapoungana lita zaidi ya milioni 6 zitakuwepo ndani ya mamlaka moja ambazo zitakidhi mahitaji ya wakazi wa wilaya hiyo.
Katika hatua nyingine ameagiza bei mpya itatozwa wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji( EWURA) ikiendelea kuchakata bei halisi itakayotozwa kwa wananchi.
Naye Mbunge la jimbo la Karatu, Daniel Awackii (Mb) amemshukuru Waziri Aweso kwa kuunganisha bodi hizo mbili na kuwa moja kwa maendeleo ya wananchi na kuongeza kuwa hivi sasa watafanya vikao na wanachi kuhusu wananchi kulipa ya bei hiyo ya unit moja kwa shilingi 1,300 kwa kila mmoja badala ya sh,2000 hadi 3000.