Home Michezo SAMIA CUP 2025 KUANZA KUTIMUA VUMBI FEBRUARY 7 KIGAMBONI, TIMU 32 KUSHIRIKI

SAMIA CUP 2025 KUANZA KUTIMUA VUMBI FEBRUARY 7 KIGAMBONI, TIMU 32 KUSHIRIKI

Mashindano ya mpira wa miguu ya Samia Cup 2025 yanayolenga kuibua vipaji na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, yanatarajiwa kuanza rasmi Februari 07, 2025, katika viwanja vya Mji Mwema, Kigamboni.

Katika hafla ya ugawaji wa vifaa kwa timu shiriki iliyofanyika leo Jumamosi Februari Mosi, 2025, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni ambaye pia ni Afisa Utamaduni wa Manispaa hiyo, Lunzegere Kilala, amewahimiza wachezaji kushiriki kwa nidhamu na malengo ya kuinua vipaji vya vijana, huku akisisitiza kuwa michezo ni fursa ya ajira kwa Watanzania.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Rashid Mfaume Suleiman, amesema mashindano hayo yameandaliwa na Taasisi ya Twende Pamoja na Mama Sports Promotion ili kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza michezo nchini.

Timu 32 kutoka Dar es Salaam zinatarajiwa kushiriki, huku mshindi wa kwanza akitarajiwa kuondoka na shilingi milioni 2, wa pili shilingi milioni 1, na wa tatu shilingi 500,000.

Mashindano hayo pia yamedhaminiwa na Makunduchi Vila Hotel, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), na Jamii Dispensary, huku ulinzi na usalama ukiimarishwa kwa ajili ya ustawi wa mashindano hayo.

Singa Peter Muga ambaye ni mwakilishi wa timu ya Mapepe FC kutoka Ubungo, amesisitiza kuwa, wamekuja Kigamboni kuonesha vipaji vyao na kushindana kwa kiwango cha juu.

Mashindano hayo yanaungwa mkono kwa karibu na Manispaa ya Kigamboni, ikishirikiana na Chama cha Soka Wilaya ya Kigamboni (KDFA) kuhakikisha ligi inafanyika kwa kuzingatia taratibu, sheria, na kanuni za mchezo.

Kwa upande wao, mashabiki na wadau wa Michezo wameeleza kuwa, wanatarajia kushuhudia ligi ya kuvutia inayolenga kukuza vipaji vya soka nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!