
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Abdallah Komba, leo Februari 28, 2025, ametembelea na kukagua ujenzi wa shule mbili za amali katika Jimbo la Geita na Busanda, Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo mikubwa katika sekta ya elimu, Mhe. Komba amesema kuwa shule hizo zitaleta mageuzi makubwa katika mfumo wa elimu wilayani humo.
“Tuna kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuleta fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa shule hizi za amali. Shule ya Sekondari ya Nzera imepatiwa Shilingi milioni 584.2, huku Shule ya Sekondari ya Amali ya Chibingo, iliyopo Kata ya Nyamigota, nayo ikipokea kiasi sawa na hicho,” alisema Mhe. Komba.

Aidha, Mhe. Komba amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ndg. Karia Rajab Magaro, kwa usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa kwa fedha nyingi kutoka Serikali ya Awamu ya Sita.
“Nampongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa usimamizi mzuri wa miradi hii, hasa ikizingatiwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina jiografia kubwa,” aliongeza.
Mhe. Komba ameeleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kuwataka wahandisi kuongeza ueledi katika usimamizi wa ujenzi tangu hatua za awali ili kuhakikisha majengo yanakuwa imara na yanadumu kwa muda mrefu.

Vilevile, ameitaka Halmashauri kuzingatia taratibu za manunuzi kupitia mfumo wa NeST katika kukamilisha miradi hiyo kwa ufanisi. Pia, amewataka mafundi kuongeza kasi ili ujenzi ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ndg. Karia Magaro, amezitaka kamati za ujenzi kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa miradi hiyo ili wanafunzi watakaotumia shule hizo wapate mazingira bora ya kujifunzia.
Shule hizo zinajumuisha:
- Madarasa 8
- Ofisi 2
- Maktaba 1
- Jengo la TEHAMA 1
- Jengo la Utawala 1
- Maabara ya Baiolojia na Kemia
- Nyumba ya mtumishi
Utekelezaji wa miradi hii ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha sekta ya elimu kwa kuwapatia wanafunzi mazingira bora ya kujifunza na kukuza ujuzi wao.