Home Kitaifa SABABU ZA HITILAFU  KWENYE MFUMO WA GRIDI YA TAIFA

SABABU ZA HITILAFU  KWENYE MFUMO WA GRIDI YA TAIFA

Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) limeeleza sababu iliyopelekea athari kwenye mfumo wa Gridi ya Taifa na kukosekana umeme kwa baadhi ya maeneo nchini ni hitilafu kwenye mfumo wa kudhibiti kiwango cha maji kwenye mitambo ya kufua umeme ya Kidatu na hivyo kushindwa kuzuia mtiririko mkubwa wa maji yanayoingia kwenye mitambo na kusababisha mitambo kujizima kwa ghafla ili kujilinda.

Hayo yameelezwa kwenye taarifa ya shirika hilo iliyotolewa na kurugenzi ya mawasiliano na uhusiano kwa umma TANESCO – Makao makuu Dodoma leo jumatatu, 01 Aprili 2024.

Aidha mitambo hiyo ya kudhibiti uingizaji maji kwenye kituo cha kidatu zilizopata hitilafu tayari zimekwisha badilishwa na kufungwa nyingine na kazi ya kutoa maji yaliyoingia kwenye vyumba vya kuendesha mitambo inaendelea pamoja na kuanza taratibu za kuwasha mitambo ya kufua umeme.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa baadhi ya Mikoa ikiwamo Iringa, Tanga, Pemba, Unguja na baadhi ya maeneo ya Dar-es-salaam na Pwani yameanza kupokea umeme kupitia mitambo ya kufua umeme ya Pangani na Ubungo Namba 2 na taratibu za kimfumo za kurejesha umeme kwenye maeneo yote zinaendelea kwa haraka

Aidha shirika hilo linawaomba radhi wateja wake wote na umma kwa ujumla kuhusu kadhia iliyojitokeza ya kukosa nishati ya umeme katika kipindi hiki cha mapumziko ya sikukuu ya Pasaka

Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko amewaelekeza viongozi wote wa Wizara, TANESCO na wafanyakazi wote waliokuwepo kwenye mapumziko ya sikuu ya Pasaka kurudi haraka kazini kuanzia muda watatizo lilipojitokeza ili kuhakikisha umeme unarejea kwenye maeneo yote.

Pamoja na maelekezo hayo Mhe. Dkt. Biteko yupo njiani kuelekea kwenye kituo cha Kidatu kuona maendeleo na jitihada zinazoendelea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!