Home Kitaifa REA YAENDELEA NA USAMBAZAJI WA MITUNGI YA GESI YA KILO SITA MKOANI...

REA YAENDELEA NA USAMBAZAJI WA MITUNGI YA GESI YA KILO SITA MKOANI KILIMANJARO

📌Mitungi ya gesi 19,530 kusambazwa mkoani Kilimanjaro

📌Kila wilaya kupatiwa mitungi ya gesi 3,255

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeingia mkataba na mtoa huduma kampuni ya Lake Gas ambaye atahudumia wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuuza kwa bei ya ruzuku mitungi ya gesi ya kilo sita pamoja na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.

Hayo yamebainishwa leo Januari 28, 2025 mkoani Kilimanjaro na Mhandisi wa miradi wa REA, Gift Kombe wakati wa ufatiliaji na usimamizi wa mradi wa ugawaji mitungi ya gesi ya kilo sita Kata ya Malangu, Wilaya ya Moshi mkoani kilimanjaro.

Mha. Kombe amesema kuwa mitungi ya gesi 19,530 itakayosambazwa mkoani kilimanjaro itachochea kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati safi na salama.

“Lengo la mradi ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji wa miti, kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi, kuboresha afya za wananchi pamoja na ustawi wao kwa ujumla”.

Mha. Kombe amesema, Serikali kupitia REA imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi (LPG) katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa mji na katika mkoa huo kiasi cha shilingi milioni 406.5 kimetengwa kutekeleza mradi huo.

Amezitaja wilaya zitakazonufaika kuwa ni pamoja na Wilaya ya Moshi, Same, Hai, Siha, Mwanga na Rombo.

Kwa upande wake, Mtendaji wa kata ya Malangu , Bw. Godlisten Lucas Johanes ameipongeza REA kwa kuja na mradi huo na kuiomba iwe endelevu ili iweze kuwasambazia wananchi wengi nishati hiyo muhimu Na kuchochea ustawi wa maisha ya wananchi na maendeleo kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!