WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umeanza usambazaji wa umeme katika vitongoji awamu ya pili (HEP II) ambapo utapeleka umeme kwenye vitongoji 135 kwenye majimbo Tisa, Mkoani Pwani kwa gharama ya sh.bilioni 14.983.7.
Mradi huu utafikia vitongoji 15 katika kila jimbo Mkoani humo na unatekelezwa na mkandarasi M/s China Railway Construction Electrification Bureau Co.Ltd .
Akimtambulisha mkandarasi wa mradi huo kwa mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Jones Olotu, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini (REA), alieleza mkoa huo una jumla ya vitongoji 2,045 ambapo vitongoji 1,135 vimeshapatiwa umeme sawa na asilimia 55.6.
Aidha vitongoji 135 kati ya 910 vilivyosalia vitapatiwa umeme kupitia mradi wa vitongoji vya majimbo.
“Vitongoji 22 vimepatiwa umeme kupitia mifumo ya umeme wa jua (solar) kwa kuwa vipo maeneo ya visiwani.
Olotu anaeleza kwamba, vitongoji 753 vilivyobakia vitaendelea kupatiwa umeme kupitia miradi ya umeme vitongojini kulingana na upatikanaji wa fedha.
Kadhalika alifafanua, REA inaendelea na utekelezaji wa miradi minne yenye thamani ya zaidi ya bilioni 59 na wakandarasi waendelea na majukumu yao.
Nae Mkuu wa mkoa wa Pwani,alhaj Abubakar Kunenge, aliagiza taarifa hizo zifikishwe kwa wakuu wa wilaya zote Mkoani hapo ili waweze kusimamia kulingana na vitongoji vilivyoelekezwa.
Vilevile aliwataka wakandarasi kutekeleza mradi kwa viwango kulingana na mikataba yao na kukamilisha kwa wakati.
“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuufungua mkoa wa Pwani kuwa mkoa wa kimkakati, kwa kuleta miradi mingi ikiwemo ya huduma ya umeme,maji, miundombinu ya barabara” alieleza Kunenge.
Ofisa Usalama na afya mahali pa kazi kutoka kampuni ya mkandarasi (CRCEBLT) Felister Lusuve waliahidi kwenda kufanya kazi kwa ufanisi kama walivyofanya katika mradi wa REA III mzunguko wa pili.
Mwisho