-Aiombea ushindi dhidi ya Pan kesho
Na Shomari Binda-Musoma
MKUU wa mkoa wa Mara Said Mtanda amesema anajipanga kutafuta milioni 30 kwaajili ya kutoa motisha kwa wachezaji na bechi la ufundi kwa timu ya Biashara United.
Kiasi hicho amekusudi kutenga shilingi milioni 2 kwa michezo 15 ya mzunguko wa pili kwenye ligi ya Champion ili kuweka hamasa zaidi ya ushindi.
Akizungumza na Mzawa Blog kwa njia ya simu amesema fedha hizo atawashirikisha wadau mbalimbali wa soka wa mkoa wa Mara waliopo ndani na nje ya mkoa.
Mtanda amesema mkoa ukiwa na timu ya ligi kuu una changamka na shughuli za kiuchumi zinafanyika zikiwemo za wajasiliamali.
Amesema kila mmoja aone kuwepo kwa ligi kuu ni fursa hivyo ni muhimu kuhakikisha timu hiyo inarejea ligi kuu.
“Ni muhimu kuongeza hamasa kwa vijana kwenye kila mchezo wa mzunguko wa pili na kila mdau awe tayari kuwezesha jambo hili lifanikiwe”
“Tunataka kuwa na mipango madhubuti kuhakikisha tunarejea ligi kuu na moja ya mpango ni kuongeza hamasa na motisha kwa wachezaji” amesema RC Mtanda.
Mkuu huyo wa mkoa amewataka wachezaji kupambana kwenye mchezo wa kesho jumatatu dhidi ya Pan Africa ili kuweza kushinda mchezo huo.
Amesema matokeo ya pointi 3 yataongeza muelekeo nzuri kabla ya kuanza mzunguko wa pili baada ya mchezo huo utakaofanyika kwenye uwanja wa Karume mjini Musoma