Na Shomari Binda-Musoma
MKUU wa mkoa wa Mara Said Mtanda amepokea kwa shangwe ushindi wa timu ya Biashara United wa mabao 3-1 dhidi ya Transit Camp.
Ushindi huo ni mfululizo wa mechi 3 za ushindi katika ligi ya Championship inayoendelea kushika kasi.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mzawa Blog mara baada ya kupokea matokeo hayo Mtanda amesema vijana wanastahili pongezi kutokana na matokeo hayo.
Amesema ligi ya Championship ni ngumu na matokeo ya pointi 3 yana maana kubwa kwa kuwa yanaiweka timu kwenye nafasi nzuri.
Mtanda amesema mkoa utaedelea kutoa sapoti kwa timu kwenye kila mchezo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kurudi ligi kuu.
“Nimepokea matokeo ya ushindi wa Biashara United kwa shangwe kubwa kwa kuwa ni ushindi wa 3 mfululizo”
“Nawapongeza wachezaji benchi la ufundi na mashabiki wote kwa ushindi tuliopata na tutaendelea kufanya vizuri” amesema Mtanda.
Kwa upande wake kocha wa timu ya Biashara United Amani Josia amesema ushindi huo unazidi kuwaimalisha katika msimamo wa ligi.
Amesema wataendelea kukitengeneza kikosi ili kiendelee kufanya vizuri na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kurejea ligi kuu msimu ujao.