Home Kitaifa RC MTAMBI AONGOZA MAJADILIANO UELEKEO DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2025-2050

RC MTAMBI AONGOZA MAJADILIANO UELEKEO DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2025-2050

MKUU wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi ameongoza majadiliano yaliyohusisha wananchi na viongozi kuelekea maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2026-2050.

Akizungumza kwenye kikao maalum cha kamati ya ushauri ya mkoa ( RCC ) kilichofanyika leo agosti 19 kwenye ukumbi wa uwekezaji amesema tayari majadiliano hayo yamefanyika ngazi ya wilaya na sasa ni mkoa kabla ya kupelekwa maoni ngazi ya taifa kwenye tume ya mipango.

Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ni suala la msingi katika masuala mbalimbali hivyo mkoa unayo nafasi kwa wananchi na viongozi kujadiliana

Mtambi amesema lengo la kikao hicho ni kutoa fursa kwa wananchi na viongozi wa mkoa wa Mara kutoa maoni yao kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 ambayo ipo katika hatua za maandalizi.

“Dira inaonyesha matamanio na vipaumbele vya wananchi,serikali na taasisi binafsi zinapo tamani kufikia kwa muda flani na mipango mbalimbali inawekwa ili kufikia lengo hilo”

“Mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ulizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango April, 2024 mkoani Dodoma ns Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni amezindua ushirikishwaji wa wadau wote kutoa maoni”, amesema.

Kanali Mtambi amesema Tume ya Mipango imewasilisha katika Mkoa wa Mara maelekezo ya namna ya kukusanya maoni, mapendekezo na ushauri ili wananchi, viongozi na taasisi zitoe maoni kwa ajili ya dira mpya ya maendeleo ya Taifa kwa miaka 25 ijayo.

Amesema kwa kawaida Nchi inakuwa na mipango ya muda mrefu, muda wa kati na muda mfupi na utekelezaji wake unaweza kulitoa taifa kutoka katika eneo moja kwenda eneo lingine.

Mkuu huyo wa mkoa amesema anatamani katika mipango ya miaka ijayo reli ya kisasa ya SGR iwe imefika mkoa wa Mara kutokea Arusha au Mwanza ili kurahisisha usafiri kwa watu na mizigo kutoka katika mkoa wa Mara na kuinua uchumi.

Akizungumza katika kikao hicho Naibu Waziri wa Sheria na Katiba Jumanne Sagini amesema mkoa wa Mara umepiga hatua kubwa katika miundombinu ya barabara ambapo hapo awali wananchi walikuwa wanatumia zaidi usafiri kupitia nchi za Kenya na Uganda wakati wa kwenda Dar es Salaam na mikoa mingine.

Sagini ameshauri mkoa utilie mkazo kuhusu urejeshaji wa bandari ya Musoma ili iweze kufanya kazi kuunganisha na treni ya SGR ambayo inatarajiwa kufika mkoa wa Mwanza na hivyo itasaidia katika usafirishaji wa mizigo na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa.

Naibu Waziri huyo amesema tayari serikali imeshajenga meli nyingi na inaendelea kujenga nyingine na hivyo inawezekana bandari ya Musoma ikifufuliwa itasaidia katika kuimarisha usafiri wa mizigo na kuvutia wawekezajai zaidi katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Sagini amesema katika sekta ya elimu nchi imepiga hatua kubwa sana tumepanuka sana, walimu wapo wachache, walimu na wazazi tunaowajibu kuhakikisha wanafunzi wanasoma.

Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo amesema wakati taifa linatoa maoni ni vizuri wataalamu wa mipango wakajiuliza wakati huo Dira inapotekelezwa Tanzania itakuwa na watu wangapi, dunia pia itaakuwa na watu wangapi ili kupanga mipango yenye uhalisia.

Prof. Muhongo amesema katika mwaka wa 2050 Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 120 hadi 141ambao ni zaidi ya mara mbili ya watu waliopo sasa na mipango yote inatakiwa kuwekwa kwenye mahesabu watu hao ili Tanzania isipange mipango kwa ajili ya watu wachache wakati inakadiriwa kutakuwa na watu wengi.

Amesema idadi ya watu ni muhimu kwa ajili ya kuangalia maendeleo tunayoyahitaji ni kwa ajili ya kuhudumia watu wangapi na kama mipango ya Taifa inaendana na idadi hiyo ya watu wanaotegemewa kuwepo wakati huo.

Ametolea mfano wa umeme na kusema kuwa kwa sasa umeme unatosheleza kwa kuwa bado idadi ya watu na viwanda na maofisi ni ndogo ukilinganisha na wakati huo na kutahadharisha kuwa ili kuwa na umeme wa uhakika wa wakati huo ni lazima kuangalia mahitaji halisi ya umeme kwa wakati huo na sio hali ya sasa hivi tu.

Aidhavwashiriki wengi wamepongeza maendeleo yaliyofikiwa katika sekta mbalimbali hapa nchini na kuitaka serikali kuendelea kuimarisha utendaji kazi katika utumishi wa umma ili maendeleo yaweze kufikiwa kiurahisi zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!