Home Kitaifa RC MTAMBI AAGIZA WANAFUNZI WOTE WANAPATA CHAKULA SHULENI IFIKAPO JANUARI 2025

RC MTAMBI AAGIZA WANAFUNZI WOTE WANAPATA CHAKULA SHULENI IFIKAPO JANUARI 2025

Na Shomari Binda-Musoma

MKUU wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi ameagiza wanafunzi wote wanapata chakula shuleni ifikapo januari 2025.

Kauli hiyo ameitoa leo septemba 19 alipokuwa akiongoza kikao cha viongozi na watendaji wa mkoa wa Mara kuhusu utoaji wa chakula shuleni na kuwataka viongozi, wazazi na wadau kuhakikisha wanafunzi wote wa mkoa wa Mara wanapata chakula cha mchana shuleni kuanzia januari, 2025.

Amesema viongozi wa serikali wa mkoa wa Mara wanapaswa kusimamia maelekezo hayo na kuhakikisha wanafunzi wote wanapata angalau mlo mmoja wa mchana wakiwa shuleni ili waweze kujifunza vizuri.

Kanali Mtambi amesema chakula kwa wanafunzi kina umuhimu mkubwa kumfanya mwanafunzi kuelewa kile anachofunfishwa na walimu akiwa darasani.

Amesema katika zoezi hilo wazazi na walezi washirikishwe ili kuhakikisha unawekwa utaratibu mzuri unaeekwa wa wanafunzi kupata chakula hicho.

“Haikubaliki kuendelea kuwafanyia ukatili wanafunzi kwa kuwashindisha na njaa kwa sababu tu viongozi na wazazi tumeshindwa kutimiza wajibu wetu katika kutoa chakula shuleni.

” Twendeni tukatekeleze agizo hili na kuhakikisha ifikapo januari 2025 wanafunzi wanapata angalau mlo mmoja wakiwa shuleni”,amesema.

Amesema kinachochangiwa sio cha ziada bali ni chakula ambacho mtoto akiwa nyumbani angekula na hivyo ni wajibu wa wazazi na walezi wa wanafunzi kutoa chakula hicho ili wanafunzi wapate chakula wakiwa shuleni.

Aidha mkuu huyo wa mkoa amezitaka halmashauri kuhakikisha kuwa shule zote zenye maeneo au mashamba zitumie maeneo hayo kulipa na kupata chakula ili kuwasaidia wazazi katika mchango wa chakula na kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo kuhusu kilimo na shughuli za kujitegemea na kutaka halmashauri kuunda sheria ndogondogo juu ya agizo hilo.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bi. Judith Mrimi amesema programu ya chakula shuleni ni muhimu kwa ajili ya kuongeza udahili na usajili wa wanafunzi, mahudhurio, usikivu na kuinua ufaulu wa wanafunzi katika mitihani.

Amesema kwa mujibu wa mwongozo wa Kitaifa wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi wa elimu ya msingi wanafunzi wote wa shule za kutwa za msingi na sekondari wanapaswa kupata huduma ya chakula cha mchana shuleni.

Ameongeza kuwa mwongozo huo umebainisha kuwa chakula kwa ajili ya wanafunzi kitapatikana kutoka kwa serikali kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na kwa shule za kutwa michango ya chakula itatoka kwa wadau wa elimu, sekta binafsi, wabia wa maendeleo, mashamba na bustani za shule namichango ya wazazi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!