Home Kitaifa RC KATAVI AWAHAKIKISHIA WAFANYABIASHARA MAJIMOTO MAZINGIRA WEZESHI

RC KATAVI AWAHAKIKISHIA WAFANYABIASHARA MAJIMOTO MAZINGIRA WEZESHI

Na:OMM- Katavi

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe.Mwanamvua Hoza Mrindoko amewahakikishia Wafanyabiashara wa kuchakata Mazao katika eneo la Majimoto Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe kuwa Serikali inayo dhamira ya dhati ya kujenga Mazingira wezeshi kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji katika eneo la Majimoto ikiwa ni pamoja na kuboresha Miundombinu ya Barabara pamoja na upatikanaji wa Nishati ya Uhakika katika eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa Mrindoko amewaeleza Wafanyabiashara na Wawekezaji dhamira hiyo ya Serikali 29 Desemba 2022 katika Ziara yake Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe alipotembelea Maghala ya Chakula kujiridhisha uwepo wa chakula cha kutosha katika Eneo hilo ambapo pia alipata fursa ya kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili Wafanyabishara hao.

Ninafahamu kuwa bado tuna matatizo yanayohitaji uboreshaji zaidi wa Barabara zetu,Tuna barabara inayotoka majimoto kwenda Inyonga na barabara ile ni ya kiwango cha changarawe hivyo ni changamoto wakati wa Mvua.Ninayo Habari njema kwenu kuwa tayari Barabara ile inafanyiwa usanifu ili kuiwezesha Serikali kutafuta Fedha kwa ajili ya Ujenzi wa Barabara hiyo kutoka Majimoto kwenda Inyonga kwa Kiwango cha Lami”Alisema Mkuu wa Mkoa Mrindoko.

Aidha Mhe.Mrindoko ameeleza kuwa Serikali chini ya Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa sasa inaendelea na Ujenzi wa Barabara ya Kibaoni kwenda Sitalike Mpanda kupitia Hifadhi ya Taifa Katavi kwa Kiwango cha Lami ambapo tayari Serikali imetoa Fedha kwa Mkandarasi kwa ajili ya Ujenzi wa Kilomita 50 na tayari Mkandarasi huyo ameanza Ujenzi wa Barabara hiyo.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa Ujenzi wa Barabara hizo kwa kiwango cha Lami kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufungua Milango ya Biashara katika eneo hilo pamoja na kuchochea ukuaji wa Uchumi katika eneo hilo.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Mrindoko amewahakikishia Wafanyabishara hao kuwa Serikali inafuatilia na inachukua hatua madhubuti ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto ya Nishati katika eneo hilo ambapo hatua ya Serikali kutoa Fedha kiasi cha zaidi ya Shilingi Bilioni 60 kwa ajili ya Umeme wa Gridi ya Taifa utamaliza kabisa changamoto ya Umeme kukata mara kwa mara jambo litakalowezesha Viwanda kufanya kazi muda wote kwa uhakika zaidi.

Akiwa Majimoto Mkuu wa Mkoa Mhe.Mwanamvua Mrindoko pamoja na shughuli nyingine alitembelea Kiwanda cha kuchakata Mazao cha Mfanyabiashara almaarufu Mtemi,pamoja na Kiwanda cha Kuchakata Mazao ya Nafaka cha Mfanyabiashara Mwanamama almaarufu Mama zai.

Eneo la Maajimoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Wilayani Mlele linavyo zaidi ya Viwanda 200 vya kuchakata Mazao mbalimbali ya Nafaka ambapo Wafanyabiashara mbalimbali kutoka ndani na Nje ya Nchi hufika Majimoto kwa ajili ya kuchukua Mazao mbalimbali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!