Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Albert Chalamila amekagua uwanja wa ndege wa Dar es Salaam Terminal I eneo ambalo ndilo viongozi na wageni mashuhuri huwasili ili kuangalia maandalizi ya kupokea Marais wa nchi washiriki wa mkutano huo, Wageni na wadau mbalimbali wa sekta ya Nishati watakaowasili nchini ili kushiriki mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu Nishati unaotarajiwa kufanyika Januari 27 na 28, 2025 kwenye ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mkutano huu umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kamisheni ya Umoja wa Afrika, na Serikali ya Tanzania.
Lengo kuu la mkutano huu ni kujadili na kuchagiza upatikanaji wa nishati ya uhakika na nafuu barani Afrika, kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Takwimu zinaonyesha kuwa takriban Waafrika milioni 685 hawana huduma ya umeme; hivyo, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika wameanzisha mpango maalum uitwao “Mission 300,” wenye lengo la kuwafikishia umeme Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.
Katika mkutano huu, nchi 14 zitakazoshiriki zinasubiriwa kusaini Mpango wa Nishati, ambao ni ahadi ya serikali zao kuchukua hatua mbalimbali za kufikisha umeme kwa wananchi. Nchi hizo ni Tanzania, Liberia, Senegal, Niger, Nigeria, Chad, Mauritania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Côte d’Ivoire, Burkina Faso, Malawi, Msumbiji, na Zambia.
Tanzania ilichaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu kutokana na mipango yake thabiti ya kusambaza umeme nchi nzima, ikiwa ni pamoja na vijiji na vitongoji, pamoja na juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Malengo ya Tanzania ni kuhakikisha asilimia 75 ya wananchi wamefikiwa na umeme ifikapo mwaka 2030, na asilimia 80 wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Mkutano huu ni fursa muhimu kwa nchi za Afrika kujadili mikakati ya pamoja ya kuongeza upatikanaji wa nishati, ambayo ni msingi wa maendeleo endelevu na ukuaji wa uchumi barani Africa.