![](https://www.mzawa.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250207-WA0212.webp)
Na Shomari Binda – Musoma
MKURUGENZI wa Hoteli ya Le Grand Victoria ya mjini Musoma, Ramadhani Msomi, amewapongeza viongozi wa kundi la WhatsApp la Jamii ya Wana Musoma kwa juhudi zao za kuendelea kuwaunganisha watu na kusaidiana katika nyakati za shida.
Kauli hiyo ameitoa kwa niaba ya wanajamii hao alipokuwa akishiriki kwenye makabidhiano ya rambirambi kwa familia ya Selemani Keraba, mmoja wa wanajamii, kufuatia msiba wa mama yake mzazi.
Msomi amesema viongozi hao wamefanya kazi kubwa ya kuunganisha jamii kwa kipindi cha miaka minane, na amesisitiza kuwa kazi hiyo inapaswa kuungwa mkono ili iweze kuendelea.
“Ninawashukuru viongozi wa kundi hili kwa juhudi zenu za kuwaunganisha watu wa Musoma, hasa kwa kipindi cha miaka hii minane. Sio kazi rahisi kuwasimamia watu, kukusanya michango yao, na kuhakikisha hakuna lawama yoyote inayotokea. Hii ni ishara ya uadilifu na uwajibikaji,” alisema Msomi.
Ameongeza kuwa kama wanajamii, wanapaswa kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wao, na yeye binafsi atahakikisha anaendelea kuwaunga mkono katika kila jambo litakalokuja mbele.
“Viongozi wa jamii ya Musoma, niwashukuru kwa kazi nzuri mnayoifanya, hata tunapokuwa mbali na Musoma, juhudi zenu zinatusaidia kuungana na kusaidiana. Ni muhimu kuendelea kuunga mkono juhudi hizi,” alisema Msomi.
Akipokea mchango wa rambirambi wa shilingi milioni 3,600,000 kwa niaba ya familia ya mfiwa, Mwenyekiti wa kundi la Jamii ya Wana Musoma, Benedict Magiri, amewashukuru wanajamii wote waliochangia, na kusema kuwa lengo la kundi ni kufanikisha miradi mikubwa zaidi, licha ya kumaliza harambee ya rambirambi.
Amesema kundi lina mipango ya kupanua shughuli zake kwa kupata viti 500, mab tents manne, na vyombo vya matangazo. Hizi ni sehemu ya malengo ambayo kundi linakusudia kuyatekeleza kupitia harambee itakayofanyika Februari 21, na amewaomba wanajamii na wadau kuchangia ili kufanikisha makusudi hayo.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Selemani Keraba amewashukuru wanajamii kwa msaada na faraja waliyompa wakati wa msiba wa mama yake mzazi.
Mweka Hazina wa kundi hilo, Ismail Massaro, ametoa ufafanuzi kuhusu utaratibu wa michango ya kundi hilo, na kusema kuwa wanachama wanaostahili kuchangia ni wale waliokuwa na michango ya misiba mitatu mfululizo.
Aidha, Massaro amewakumbusha wanajamii kuchangia harambee hiyo itakayofanyika Februari 21 kabla ya tarehe ya mwisho ya kuchangia, Februari 15, kwani michango hiyo ni sehemu ya vigezo vya kusaidiwa.
![](https://www.mzawa.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250207-WA0211.webp)