Home Kitaifa RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFUNGUA MKUTANO WA SIKU TATU WA AFCTA WA...

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFUNGUA MKUTANO WA SIKU TATU WA AFCTA WA WANAWAKE KUTOKA NCHI MBALIMBALI

Na Magrethy Katengu

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema nchi za Afrika zinapaswa kuwekeza katika rasilimali watu hususan elimu kwa vijana ili kuwa na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Sambamba na hayo, amesema maendeleo ya bara la Afrika yatapatikana haraka iwapo wanawake na vijana watawezeshwa kwa mitaji na taasisi za fedha pamoja na kuwaondolea vikwazo vya kibiashara hasa katika maeneo ya mipakani.

Samia alisema hayo jana wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) katika Ukumbi wa Mikitano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.


Mkutano huo wenye kaulimbiu “Wanawake na Vijana: Injini ya Biashara ya AfCFTA Barani Afrika” ni wa kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.

Alisema Afrika inahitaji nguvu kazi imara katika maendeleo ya kiuchumi hivyo uwekezaji katika elimu kwa vijana ni muhimu kwa kuwa sababu kubwa ya nchi nyingi zilizopiga hatua kimaendeleo ziliwaendeleza vijana kielimu.

Rais Samia alitoa mfano wa China ambayo alisema maendeleo yake yanachangiwa na kuwa na vijana wenye ujuzi hasa katika sayansi na teknolojia, hivyo nchi za Afrika hazina budi kuwekeza kwa vijana katika elimu ikiwamo ubinifu katika nyanja mbalimbali.

“China ni nchi ambayo inapigiwa mfano kwa maendeleo na siri kubwa ni uwekezaji iliyofanya ka vijana. Kampuni nyingi zinazofanya vizuri zinaongozwa na vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 pamoja na matumizi ya sayansi na teknolojia Afrika inaweza pia kujenga uchumi imara kwa kuwekeza zaidi kwa vijana katika elimu hasa sayansi. Kwa kufanya hivi tutapiga hatua kubwa kiuchumi,”alisema.

Pia alisema njia nyingine katika kufikia malengo ya maendeleo ni kuondoa vikwazo vinavyowakabili wanawake na vijana. Sambamba na hiyo, alisema mabadiliko ya kisera na kisheria yanapaswa kufanywa ili kutimiza azma hiyo.

“Wanawake na vijana wanakumbana na vikwazo mbalimbali katika biashara zao hasa maeneo ya mipakani hasa mambo ya leseni na vibali. Tunashukuru kwa Afrika Mashariki tumepunguza tatizo hili kwa kiasi kikubwa, hivyo ni changamoto kwetu kuanzia maeneo ya kikanda na baadaye bara zima la Afrika kuondoa vikwazo hivi,” alisema.

Rais pia alisema Tanzania imeanza kuondoa vikwazo mbalimbali ambavyo vinawakwamisha wanawake na vijana katika biashara na masuala mengine ya maendeleo vikiwamo ukosefu wa mikopo yenye masharti na riba nafuu kutoka taasisi za fedha, sera na ubaguzi na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake.

“Katika masoko kwa mfano tumebaini kwamba hakuna maeneo ambayo wanawake wanaweza kutunzia watoto wakati wanafanya biashara na tumeanza kulitafutia ufumbuzi hili. Mwanamke anabeba mtoto kutwa nzima akiwa sokoni anafanya biashara, hili si zuri.
Lakini pia suala la usawa wa kijinsia katika biashara linafanyiwa kazi. Kuna unyanyasaji wa kijinsia katika biashara kwamba baadhi ya kazi ni za wanaume tu pia wanawake wamepewa majina mabaya ambayo ni unanyasaji,” alisema.

Kuhusu ununuzi wa umma, alisema serikali imeanza kutekeleza mpango wa kuziwezesha kampuni za vijana na wanawake kutoa huduma serikalini. Alisema lengo ni kufikia asilimia 30 ya kampuni zinazomilikiwa na wanawake na vijana kutoa huduma hizo.

“Kuna miradi mingi ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara vijijini. Asilimia 30 au zaidi ya kazi hizi tutatoa kwa wanandishi na makandarasi wanawake ikiwa uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na kuleta maendeleo endelevu,” alisema.

Rais Samia alisema Afrika pia inatakiwa kutumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya kujiletea maendeleo. Alizitaja baadhi ya rasilimali hizo kuwa ni maliasili, madini, mifugo, ardhi kwa ajili ya kilimo.

Alisema Afrika ina utajiri wa rasilimali lakini ni bara lenye watu wengi maskini kwa sababu rasilimali zilizopo hazitumiki ipasavyo badala yake zinanufaisha watu wa nje, hivyo wakati umefika wa kutzitumika kwa maendeleo yake.

Katika muktadha wa uwezeshaji wanawake na vijana, Rais alisema fursa hizo zinapaswa kutumiwa kikamilifu na makundi hayo ili kuleta maendeleo endelevu hususan katika uongezaji wa thamani.

Rais pia alisema nchi za Afrika zinatakiwa kuainisha fursa za kisera zitakazowawezesha wanawake na vijana kunufaika ipasavyo katika soko la ndani, kikanda na kimataifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!