Home Kitaifa RAIS WA GUINEA BISAU KUZURU TANZANIA SIKU TATU KUANZIA JUNI 21-23, 2024

RAIS WA GUINEA BISAU KUZURU TANZANIA SIKU TATU KUANZIA JUNI 21-23, 2024

Na Magrethy Katengu— Dar es salaam

Rais wa Jamhuri ya Guinea Bissau ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Muungano wa Viongozi wa Afrika katika Kudhibiti Malaria (ALMA), Mheshimiwa Umaro Sissoco Embaló anatarajia kufanya ziara ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 21 hadi 23 Juni 2024.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Juni 20, 2024 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt Samweli Shelukindo amesema ziara hiyo inalenga kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Guinea Bissau na kuibua maeneo ya ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati ikiwemo uzalishaji wa zao la korosho, masuala yanayohusu udhibiti wa ugonjwa wa Malaria kupitia Taasisi ya ALMA, na mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Hata hivyo Katibu amebainisha kuwa kupitia ziara hiyo Tanzania na Guinea Bissau zimedhamiria kuimarisha na kuinua kiwango cha ufanyaji biashara na uwekezaji hususan kupitia Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) nchi zote mbili zimeridhia.

“Ziara hii itatoa fursa kwa nchi hizi mbili kujadili kwa kina namna ya kuendelea kupambana na kudhibiti ugonjwa hatari wa Malaria kwa kuzingatia kuwa, Mhe. Rais Umaro Sissoco Embaló ni Mwenyekiti wa ALMA taasisi ambayo ilianzishwa mwaka 2009 na Viongozi wa Nchi zote 55 za Afrika kwa lengo la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030” amesema Balozi Dkt Shelukindo

Hivyo itakumbukwa kuwa, wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwaka 2023, Mwenyekiti wa ALMA, Mhe. Rais Umaro Sissoco Embaló alizitambua nchi 7 ikiwemo Tanzania kwa kubuni matumizi bora ya Kadi ya Alama ya ALMA (ALMA Scorecard) inayosisitiza uwajibikaji na kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya ugonjwa wa Malaria ambapo kupitia mpango huo, Tanzania ilitoa mafunzo kwa Wabunge, Viongozi mbalimbali na watoa huduma za Afya kuhusu namna ya kutumia kadi hiyo ya alama katika kuhamasisha uwajibikaji na utoaji elimu kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Balozi Dkt Shelukindo amesema kuhusu uzalishaji wa zao la Korosho, Guinea Bissau imejikita katika uzalishaji wa zao hilo ambalo nchi hiyo huuza zaidi nchini India ambapo thamani ya uuzaji nje wa zao hilo inafikia takribani asilimia 90 na katika nchi yao zao hilo ni chanzo kikuu cha mapato kwa wakulima wadogo wa nchi hiyo kwa asilimia 80 na huchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa la Guinea Bissau.

Hivyo inatarajiwa kupitia ziara hiyo suala la uzalishaji wa zao la Korosho ambalo pia hulimwa hapa nchini hususan katika mikoa ya Kusini ikiwemo Mtwara na Lindi litajadiliwa kwa kina.

Sanjari na hayo ziara yake, Mheshimiwa Rais Umaro Sissoco Embaló na ujumbe wake watawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba tarehe 21 Juni 2024.

Pia Mheshimiwa Rais Embaló atapokelewa rasmi Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 22 Juni 2024 na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya mapokezi hayo, viongozi hao watakuwa na mazungumzo ya faragha na baadaye watashiriki katika mazungumzo rasmi kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na Guinea Bissau, na baadaye kuzungumza na Waandishi wa Habari kuelezea masuala muhimu yaliyojiri katika mazungumzo yao.

Aidha, Mheshimiwa Rais Embaló na ujumbe wake atatembelea Miundombinu ya Reli ya Kisasa katika Kituo cha Stesheni jijini Dar es Salaam, Mamlaka ya Eneo Huru la Uwekezaji kwa Mauzo Nje (EPZA) na Taasisi ya Muungano wa Viongozi wa Afrika katika Kudhibiti Malaria (ALMA).

Aidha Ziara hiyo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na nchi mbalimbali ili kuinufaisha nchi kiuchumi ikiwa ni utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi kwa vitendo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!